Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Geita.
Kata
ya Makurugusi iliyopo katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita imeunda
vikundi mbalimbali vinavyofanya kazi katika maeneo ya migodi ili kuzuia
ajira za watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kufanya kazi katika
migodi hiyo.
Hayo
yamesemwa na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, James Masai alipokua akiongea
na waandishi wa habari juu ya Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na
Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na shirika la plan International
ulivyowasaidia wananchi wa kata hiyo.
Masai
amesema kuwa shughuli za maendeleo zinazofanywa na shirika hilo katika
kata anayoiongoza zimeleta maendeleo makubwa hasa kwenye suala la
uondoaji wa ajira za watoto katika migodi kwa kuwapatia mafunzo
mbalimbali kuhusu athari za ajira hizo.
“Katika
Kata hii tumebahatika kuwa na vituo viwili vya migodi ambavyo hapo
mwanzo watoto wengi walikua wakifanya kazi ili kujipatia vipato lakini
baada ya shirika hili kutoa mafunzo yanayohusu athari za ajira kwa
watoto kwa kila kijiji, tukaamua kuunda vikundi katika migodi hiyo ili
kukomesha kabisa suala hili”, alisema Masai.
Amefafanua
kuwa baada ya kupatiwa elimu na shirika la Plan International waliweza
kuunda vikundi ndani ya migodi hiyo vikiwemo vya kamati za ulinzi,
kamati za kutetea haki za binadamu pamoja na kamati za utawala ambazo
zinasaidia kuhakikisha usalama wa migodi ikiwa ni pamoja na kuzuia ajira
za watoto katika migodi hiyo.
Aidha,
ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kutoa elimu bure kwani hapo
mwanzo watoto walikua wakifanya kazi migodini kwa ajili ya kutafuta
fedha za kuwawezesha kulipia ada hivyo, elimu bure imewasaidia watoto
wengi kuachana na ajira za migodini na kurudi shuleni.
Naye
Mchimbaji wa madini, Samson Marwa amesema kuwa kwa sasa wanaelewa
athari za ajira kwa watoto hivyo wanashirikiana na wananchi kwa hali na
mali kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayefanya kazi katika mgodi huo.
“Sisi
wachimbaji wa madini tunashirikiana na wananchi katika kuzuia ajira za
watoto katika mgodi wetu, tunashukuru kwa kuwa tumeweza kuzuia ajira
hizo na mpaka sasa hakuna mtoto yoyote anayefanya kazi mgodini hapa”,
alisema Marwa.
0 comments:
Post a Comment