Home » » MAMA AJINYONGA BAADA YA MTOTO WAKE KUKOSA HUDUMA

MAMA AJINYONGA BAADA YA MTOTO WAKE KUKOSA HUDUMA

Na Victor Bariety, Geita
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamke mmoja amekutwa amefariki dunia, baada ya kujinyonga ndani ya eneo la Hospitali ya Wilaya ya Geita, mkoani Geita.

Mwanamke huyo, alijinyonga nje ya wodi namba moja aliyokuwa amelazwa mwanaye wa kiume, anayedaiwa kufariki kwa kukosa huduma za matibabu.


Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka hospitalini hapo, mwanamke huyo, Monika Mapoli (22) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Isima, inadaiwa alifikia uamuzi wa kujinyonga, baada ya kifo cha mtoto wake, Jumanne Philimon, mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi, kwa kukosa matibabu.


Mwanamke huyo, aligunduliwa jana akiwa amekufa huku amening'inia kwenye moja ya miti iliyopo ndani ya uzio wa hospitali hiyo.


Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Leonard Paul, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.


Alisema mtoto huyo, alipoteza maisha kwa kukosa huduma za matibabu.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Nelson Bukuru, alisema tukio hilo lilitokea saa 7 usiku wa kumkia jana.


Alisema mwanamke huyo, alifika hospitalini Agosti mosi, mwaka huu, akiwa na mtoto wake aliyekuwa akisumbuliwa na homa kali ya mapafu na pumu.


Mbali na kukanusha madai ya baadhi ya watu, waliodai mtoto huyo alifariki kwa kukosa huduma, Dk. Bukuru alikiri hospitali hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa dawa mbalimbali.


Kwa mjibu wa vyanzo vya uhakika, mtoto huyo alifariki dunia kwa kukosa matibabu, licha ya mama wa mtoto kuomba msaada kwa wauguzi waliokuwa zamu.


"Unajua hospitali hii imebaki jina...sisi wenyewe tulishuhudia mama wa mtoto akihangaika kuomba msaada, baada ya mtoto wake kuzidiwa, lakini hakuna muuguzi hata mmoja aliyeonekana kutoa msaada," alisema mmoja wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo.


Wakati huo huo, mwanamke mmoja aliyekwenda hospitalini hapo, akiwa amevaa mavazi ambayo hayatakiwi, alijikuta katika wakati mgumu, baada ya kuzuiwa na walinzi.


Mwandishi wa habari hizi, aliyekuwa eneo la geti kuu la kuingilia hospitalini hapo, alimshuhudia mlinzi wa kampuni ya KM Security, akimzuia mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Monika.


Akizungumzia tukio hilo, la wanawake waliovaa suruali kutoruhusiwa kuingia hospitalini hapo, Dk. Bukuru alikiri kuwepo kwa utaratibu huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa