na Victor Eliud, Geita
MKURUGENZI wa shirika lisilo la kiserikali linalohudumia walemavu wa ngozi (albino) la Under The Same Sun, Vick Ntetema, amemlaumu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), kwa kufuta kesi dhidi ya watuhumiwa waliohusika kumshambulia albino.
Ntetema amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Geita, Saidi Magalula, kufuatilia kujua sababu zilizotumiwa DPP kufuta kesi ya shambulio alilofanyiwa Adamu Robert (12), mkazi wa Nyaruguguna.
Mkurugenzi huyo alitoa kauli hiyo juzi kwenye tamasha la elimu ya kupinga ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi lililofanyika katika viwanja vya mamlaka ya mji mdogo wa Geita na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji huo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, watu waliomshambulia Adamu walitoweka na vidole vyake vitatu, lakini watuhumiwa hao wameachiwa huru baada ya kesi iliyokuwa katika mahakama ya wilaya ya Geita kufutwa, Mei mwaka huu.
Kesi hiyo inadaiwa kufutwa na DPP kwa madai kuwa washtakiwa hawakuwa na kesi sambamba na ushahidi kutojitosheleza.
Ntetema alisema, pamoja na ushahidi wa waziwazi uliotolewa na Adam Robert kuhusu kushambuliwa kwake mwishoni mwa mwaka jana huku polisi wakifanya uchunguzi wa kina kubaini tukio hilo, kisha kuwakamata watuhumiwa cha kushtusha DPP alifuta kesi hiyo.
Alisema baada ya tukio hilo, polisi waliwakamata baba mzazi wa mlemavu huyo Robert Tangawizi na mama yake wa kambo baada ya Adamu kuwataja kuwa walihusika kutengeneza mazingira ya kushambuliwa kwake.
Katika tamasha hilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Saidi Magalula, aliyewakilishwa na mkuu wa wilaya ya Bukombe, Aman Mwenegoha, alitakiwa kutoa tamko kwa nini serikali inafumbia macho matukio ya albino kushambuliwa na kuuawa.
Mwenegoha alisema, serikali inalaani vitendo vya kinyama dhidi ya walemavu wa ngozi na kuahidi vitendo hivyo havitatokea tena katika mkoa wa Geita hasa katika wilaya yake ya Bukombe kutokana na kuimarika kwa ulinzi na usalama kwenye familia za albino.
Kutokana na kauli hiyo, Ntetema alimtaka mkuu wa wilaya kufuatilia kwa DPP, sababu zilizomfanya atoe amri kwa mahakama ya wilaya ya Geita kuachiwa kwa washutumiwa wa shambulio dhidi ya Adam.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment