JESHI la Polisi mkoani Geita
limethibitisha kuonekana kwa mtoto Shabani Maulidi, anayedaiwa kufufuka baada
ya miaka mitatu ya kifo chake, kilichosababishwa na kutumbukia kisimani mwaka
2011.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Kamnda wa jeshi hilo, Leonard Paulo, alisema kuwa pamoja na
kuthibitisha tukio la kuonekana kwa mtoto huyo akiwa hai bado serikali haiamini
kama ni kweli alikufa na kufufuka.
“Mimi kama kamanda wa polisi na
serikali kwa ujumla, hatuamini kama mtoto huyu alikufa na kufufuka, japo wazazi
wake wanakiri hilo. Serikali haiamini vitu kama hivyo,” alisema.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Wilaya ya Geita ambapo mtoto huyo alilazwa kwa matibabu, alisema kuwa hali yake
inaendelea vizuri na wakati wowote ataruhusiwa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi
linaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli juu ya tukio hilo kwa kushirikiana
na wataalamu kutoka hospitali ya wilaya, ambapo kwa sasa hatua inayoendelea ni
kutafuta vipimo vya vinasaba (DNA).
Katika tukio jingine,
mtoto wa miezi miwili, Edga Sizya, amefariki dunia papohapo baada ya
kupigwa kichwani eneo la paji la uso na baba yake mzazi, Sizya Kilulinda
(35) mkazi wa Bugurula.
Kamanda huyo alisema kuwa tukio hilo
lilitokea Septemba 28, mwaka huu, baada ya kutokea ugomvi kati ya baba na mama
wa mtoto huyo, Kulwa Lukas (27) kwa kile alichodai kuwa ni mke kupika ugali wa
muhogo.
Alisema kuwa hatua hiyo ilizua
ugomvi, ambapo baba wa marehemu Kilulinda aliruka na kumpiga kichwa mkewe na
bahati mbaya kichwa hicho kilimpata mwanaye kwenye paji la uso akiwa amebebwa
mgongoni na mama yake.
Kufatia tukio hilo, wananchi waliamua
kumpiga Kalulinda na kupoteza maisha na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na
uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment