Home » » VICTORIOUS CENTRE CENTER OF EXCELLENCY WAWEKA MIKAKATI KUWASAIDIA WENYE USONJI

VICTORIOUS CENTRE CENTER OF EXCELLENCY WAWEKA MIKAKATI KUWASAIDIA WENYE USONJI


Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Victorious Centre of Excellency nchini Tanzania kimesisitiza dhamira yake ya kujitolea katika kutoa matibabu ya uhuishaji na elimu kwa jamii kuhusu mahitaji maalumu kwa watoto wenye hali ya usonji hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Victorious Centre of Excellency, Sarah Laiser-Sumaye ameelezea dhamira ya kituo hicho jijini Dar es Salaam hivi karibuni kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellence.

Kupitia maadhimisho hayo wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji miti, kutoa misaada mbalimbali, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni kwenye kituo hicho, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Sarah Laiser-Sumaye alisema ongezeko la kesi za hali ya usonji nchini Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla ni jambo la kuchukua hatua mapema, huku utafiti wa hivi karibuni kutoka kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) cha nchini Marekani ukibainisha kuwa mtoto mmoja  kati ya watoto 36 wanakabiliwa na changamoto ya hali ya Usonji.

"Watoto wenye hali ya Usonji hukumbana na changamoto katika mawasiliano, kushindwa kutamka maneno vizuri, hukabiliwa na ugumu katika kupokea mafunzo ya kielimu na mara nyingi huonyesha tabia za ukorofi kupindukia," Sarah Laiser-Sumaye alieleza.

 "Changamoto hizi huongezeka zaidi kutokana na uelewa hafifu na imani za kiutamaduni zinazohusiana na changamoto ya Usonji katika ukanda wa Africa,’’.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Kituo cha Victorious Centre of Excellency na Victorious Academy vimeibuka kama alama ya matumaini na usaidizi kwa watoto wenye changamoto hiyo na familia zao. 

Kupitia matibabu yao ya uhuishaji na elimu ya mahitaji maalumu, vituo hivyo vinapambana kuleta tofauti inayokusudiwa katika maisha ya watoto hao wenye mahitaji maalumu pamoja na familia zao.

Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali za tiba ya urekebishaji (rehabilitation therapies) na shughuli za ziada kwa watoto wenye hali ya usonji nchini Tanzania kwa lengo la kuwajumuisha katika jamii kupitia juhudi makini za kujengea uelewa wa kijamii.

Katika kuthibitisha uzito na umuhimu wake, tukio hilo lilipambwa na uwepo wa wadau muhimu kutoka taasisi hizo akiwemo Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, Mkuu wa Ofisi ya Msimamizi Mkazi wa UN, Shabnam Mallick, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Frederick Sumaye.

Wengine ni  Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Umoja wa Comoro na Mkuu wa Msafara wa Kidipromasia, Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih pamoja na Mabalozi wengine kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Congo, Algeria, Namibia, Msumbiji na wengine wengi.
 
Balozi Mayende-Malepe, akizungumza kwenye tukio hilo alionyesha kutambua umuhimu wa kazi zinazofanywa na Kituo cha Victorious Centre of Excellency huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na taasisi kama hiyo ili kuinua ufahamu na kupanua muelekeo wa fikra, mtazamo na maadili ya Hayati Mandela, ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya uonevu na kusaidia watu wenye uhitaji.

"Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ni fursa kwa wananchi duniani kote kwa kutambua nguvu zao binafsi za kubadili dunia kuwa sehemu nzuri na njema ya kuishi.Kupitia ushirikiano na taasisi kama Kituo cha Victorious Centre of Excellency, tunatambua pia tunaweza kuwa sehemu ya kuinua ufahamu na kupanua muelekeo wa maadili na fikra za Mandela ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ukatili na kusaidia watu wenye uhitaji maalum," Alisema Balozi Mayende-Malepe

Umoja wa Mataifa pia ulionyesha kuguswa kwake na jitihada za Kituo cha Victorious Centre of Excellency huku ukionyesha kutambua umuhimu wa uongozi wa Nelson Mandela na umuhimu wa kukuza maadili yake na kuhamasisha watu kuwa na mchango chanya kwa jamii.

"Kila kitendo uhesabiwa hata kikiwa kidogo. Iwe ni kuchora ukuta au kusaidia kuandaa chakula, michango yetu leo ni sehemu ya jitihada kubwa ya kimataifa ya kupambana na umaskini na ukosefu wa usawa. Vitendo hivi vya huduma hata kikiwa ni kidogo athari zake chanya huenea nje kwa ukubwa zaidi.’’ Alibainisha Bi. Shabnam Mallick, Mkuu wa Ofisi ya Msimamizi Mkazi wa UN nchini Tanzania.

Hatua ya wadau hao ilikuja huku Kituo cha Victorious Centre of Excellency kikiwa kinaendela kujipambanua kama mdau muhimu sio tu katika kutoa huduma zake, bali pia kuwezesha jamii, kukuza ufahamu na kuunda jamii inayowajibika. 

Kupitia juhudi zake endelevu kituo hicho si tu kinabadilisha maisha ya watoto wenye hali ya usonji, bali pia kinawajuza wengine kufuata nyayo za Hayati Nelson Mandela, kufungamanisha dhana ya ‘Ubuntu’ (Utu) na kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia mustakabali bora kwa wote.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Frederick Sumaye (wa pili kushoto) akizungumza na washiriki wakiwemo Mabalozi wa mataifa mbalimbali nchini Tanzania, pamoja na wakurugenzi wa mashirika katika maadhimisho ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini hapa nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellency. Kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kituo hicho ikiwemo upandaji miti, utoaji wa misaada ya kijamii, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu nchini. Wanaomsikiliza ni Waanzilishi na Wakurugenzi wa kituo hicho akiwemo Bw Filbert Sumaye (Kushoto) na Bi Sarah Laiser-Sumaye (wa pili kulia) pamoja na Mchungaji Dk. Eliona Kimaro (kulia)
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Victorious Centre of Excellency, Sarah Laiser-Sumaye akizungumza na washiriki wakiwemo Mabalozi wa mataifa mbalimbali nchini Tanzania, pamoja na wakurugenzi wa mashirika katika maadhimisho ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini hapa nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellency. Kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kituo hicho ikiwemo upandaji miti, utoaji wa misaada ya kijamii, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu nchini.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa