Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu
wa Wilaya ya Chato iliyopo mkoani Geita, Shaban Ntarambe amekiri kuwa
ushirikiano wa shirika la Plan International katika kudhibiti ajira
hatarishi za watoto umefanikiwa kumaliza tatizo hilo katika Kijiji cha
Msasa.
Hayo
yamesemwa leo mkoani Geita na Mkuu huyo alipokuwa akiongea na mwandishi
wa habari hii juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na
Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na shirika la plan International jinsi
ulivyowasaidia wananchi wa Kijiji hicho.
Ntarambe
amesema kuwa ushirikiano wa Shirika hilo, jamii pamoja na uongozi wa
migodi iliyopo kwenye Kijiji hicho umesaidia katika kuhakikisha elimu ya
ajira, afya na usalama kwa watoto inatolewa, hivyo kupitia elimu hizo
wananchi wamepata uelewa juu ya athari za ajira za watoto na kujumuika
katika uzuiaji wa ajira hizo.
“Tumefanikiwa
kwa asilimia zote kuzuia ajira za watoto katika eneo hilo ambalo lina
mkusanyiko mkubwa wa wachimbaji wa madini, kimsingi ni kwa sababu ya
ushirikiano unaotolewa na shirika la Plan International kwani wanatoa
rasilimali nyingi zinazowezesha kufanikisha kuondoa tatizo hilo”,
alisema Ntarambe.
Akiongea
kuhusu suala la athari wanazopata watoto wadogo wanaobebwa na mama zao
wanaofanya kazi migodini amesema kuwa wanasaidiana na shirika hilo
katika kuwapatia elimu pamoja na mitaji ili waachane na
kazi za migodi na badala yake watafute kazi mbadala za kujitafutia
vipato ili kuwakinga watoto wadogo wasiathiriwe na kazi zinazofanyika
katika maeneo hayo.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mawasiliano wa Shirika hilo, Raymond Kanyambo
amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kutambua umuhimu wa shirika hilo na
kuahidi kuendelea kushirikiana nae katika kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi wa wilaya hiyo haswa katika masuala ya
unyanyasaji wa watoto na ukatili unaofanywa kwa wanawake.
“Shirika
letu linahusika na kutetea haki za watoto, hivyo tuliona ni vyema
kupeleka nguvu zetu katika maeneo yenye migodi kwa kuwa ni maeneo
yanayoongoza katika utoaji wa ajira za watoto walio na umri chini ya
miaka 18, mradi huu ulitekelezwa katika wilaya za Nyan’ghwale na Geita
lakini baada ya kuona mafanikio tumeamua kuiongeza wilaya ya Chato ili
kukomesha kabisa tatizo hili”, alisema Kanyambo.
Mradi
huu wa miaka mitatu una lengo la kuondoa ajira hatarishi na vitendo vya
ukatili kwa watoto wanaoishi karibu na maeneo ya migodi, umeanzishwa
Novemba 2015 na utagaharimu jumla ya Euro 1,500,000 hadi kuisha kwake.
0 comments:
Post a Comment