Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Geita
Shirika
la Misaada na Maendeleo ya Jamii (CODERT) limejipanga kuwasaidia jumla
ya wananchi 7000 wanaoishi katika mazingira magumu Mkoani Geita ili waweze kujikwamua kutoka katika lindi la umasikini linalowakabili.
Shirika
hilo ni moja ya mashirika yanayoshirikiana na Shirika la Plan
International katika kutekeleza Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na
Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na shirika la plan International kwa
kuwapatia wananchi hao vifaa pamoja na elimu ya ujasiriamali.
Hayo
yamesemwa leo Mkoani Geita na Msimamizi wa Miradi wa shirika hilo,
Edward Saramba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu njia
wanazozitumia kuwainua wazazi na vijana wa mkoa huo ili waache
kuwapeleka watoto walio na umri chini ya miaka 18 kufanya kazi katika
maeneo ya migodi.
Saramba
amesema kuwa mradi huo unaoratibiwa na shirika la Plan International
umewasaidia wananchi wa mkoani Geita kuinua maisha yao kwa kuwasaidia
kuunda vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuwapatia vifaa mbalimbali
vinavyowawezesha kujipatia vipato ambavyo vinawasaidia kuendesha maisha
yao ya kila siku.
“Awamu
ya kwanza ya mradi huu iliisha Novemba 2015 na tulifanikiwa kuwafikia
wananchi wenye mazingira magumu zaidi ya 4000 waishio katika Wilaya za
Nyan’ghwale na Geita, kwa awamu hii tumeongeza wilaya ya Chato hivyo
tumejipanga kuwafikia wananchi 7000 tukiamini kuwa kuwasaidia wananchi
hao kutapunguza ajira hatarishi kwa watoto”, alisema Saramba.
Amevitaja
baadhi ya vifaa walivyovitoa kwa wananchi wanaoishi kwenye mazingira
magumu kuwa ni mashine za kujazia upepo magari na pikipiki (compressor),
vyerehani, mabomba ya maji, mizinga ya nyuki, viti na meza kwa mama
lishe, kuwapatia wafugaji kuku pamoja na mbegu za mahindi na mpunga kwa
wakulima, zaidi ya hayo waliweza kufadhili mafunzo ya kutengeneza
baiskeli, pikipiki na cherehani.
Kwa
upande wake mmoja wa wananchi waliosaidiwa kupitia Mradi huo, Shabani
Masanja ameyashukuru mashirika hayo kwa sababu kabla ya mradi huo
kumfikia alikua na maisha magumu lakini baada ya kuanza ufugaji wa kuku
aliopewa kutoka katika shirika hilo ameona tofauti kubwa ya maisha.
“Nashukuru
sana mashirika yaliyoniwezesha kwa sababu yameninufaisha, kwa sasa
ninaweza nikauza kuku na mayai vinavyoniwezesha kusomesha watoto wangu,
kununua chakula, nimeweka umeme kwenye nyumba yangu ambao unanisaidia
kufanya ufugaji wa kisasa kwa sababu mwanzoni nilikua nikikuza vifaranga
kwa kuwawekea moto lakini sasa hivi natumia umeme kuwakuza”, alisema
Masanja.
0 comments:
Post a Comment