Imeandikwa na Halima Mlacha, Dodoma.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Selemani Jaffo amewataka
viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kuacha kuwasaidia walimu
wanaopangiwa maeneo ya vijijini kukimbia maeneo hayo na kuhamishiwa
mijini.
Jaffo alisema tabia hiyo imeshamiri na kuisababishia Wizara yake na
ile ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupata tatizo kutokana na
walimu wengi kukimbia vijijini na kuwakosesha wananchi wa maeneo hayo
huduma bora ya elimu.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Geita Mjini, Kanyasu
John (CCM), aliyetaka kufahamu Serikali ina maelekezo gani kwa walimu
wapya ili waendelee kubaki vijijini walikopangiwa badala ya kukimbilia
mijini.
Akijibu swali hilo, waziri huyo alikiri siku chache zijazo Serikali
itatangaza ajira za walimu wapya na kuwapangia maeneo ya kazi. Hata
hivyo, alisema katika ajira hizo za walimu kuna mikoa takribani sita
lazima ipewe kipaumbele kutokana na kukabiliwa na changamoto kubwa ya
walimu.
Alitaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Kigoma, Rukwa, Katavi na Geita
ambako alisisitiza kuwa Serikali itatoa maelekezo maalumu kwa walimu
wapya watakaopangiwa katika mikoa hiyo.
“Moja ya maelekezo kwao ni kwamba wakifika katika mikoa hiyo ni
lazima waende katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa wa walimu. Bahati
mbaya suala linalojitokeza inawezekana kabisa nyie waheshimiwa walimu
wengine wakipelekwa kule mnawapa vimemo warejeshwe mijini, hali hii
inasababisha maeneo ya vijijini kukosa walimu,” alisema Jaffo.
Katika swali la msingi la Kanyasu, alitaka kufahamu ni kwa nini shule
ya msingi ya wasichana Nyankumbo iliyojengwa chini ya mrafi wa Geita
Gold Mine imebaki kuwa ya kutwa badala ya bweni kama mpango wa awali
ulivyokuwa kutokana na mazingira ya wilaya ya Geita.
Akijibu swali hilo, Jaffo alisema taratibu zinazotumika kuisajili
shule kuwa ya bweni ni kwa halmashauri yenyewe kuwasilisha maombi Wizara
ya Elimu kupata kibali.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment