Utafiti ulofanywa mwaka 2009 na
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa masuala ya watoto hapa nchini ulionyesha kuwa kuna
kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto.
Hata hivyo, pamoja na kuwa ni
utamaduni wa kigeni kuripoti matukio mbalimbali kupitia namba za simu na
kwenye mitandao, matumizi ya namba 116 (Child helpline) hapa nchini
yamesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa za ukatili dhidi ya
watoto.
Kama anavyoeleza Mkurugenzi
Msaidizi wa Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, Bwana. Benedict Missari kuanzia mwezi Juni 2013 hadi
mwezi Juni 2014, Wizara hiyo ilipokea jumla ya simu 16000 kati ya
hizo1659 zilielezea ukatili dhidi ya watoto.
Kati ya simu hizo 1659, “simu 107
zilikuwa za ‘physical violence’, 23 za ubakaji, 23 za unyanyasaji
mwingine wa kingono, 69 ni za kutelekezwa, 6 za utekwaji wa watoto, 12
zilihusu mimba kwa watoto huku 21 ni za uuzwaji wa watoto kwenda maeneo
mbalimbali mfano Zanzibar na nchi za Uarabuni”.
Watoto walio na umri wa chini ya miaka 18 nchini Tanzania ni sawa na asilimia 51 ya jumla ya idadi ya wananchi wote nchini.
Matukio mengi ya ukatili dhidi
yao yamekuwa yakifanyika ama shuleni au nyumbani yakiwemo ya kubakwa,
kukeketwa, kutelekezwa, kuchomwa moto, kutumikishwa kazi chini ya umri
mdogo pamoja na ukatili mwingine wa aina hizo ambao huathiri maendeleo
ya mtoto.
Ili kukabiliana na hali hiyo,
mnamo tarehe 3 Januari, 2013 Serikali chini ya Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Asasi isiyokuwa ya
Kiserikali ya C-Sema chini ya Child Helpline International(CHI)
ilianzisha na kuendesha mtandao wa mawasiliano ya simu katika maeneo ya
majaribio (Pilot Areas) katika wilaya sita ambazo ni Wilaya/Manispaa za
Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu na Hai ili kupata
taarifa za ukatili wa watoto kwa kupiga simu bure kwa kutumia namba
116(Child helpline).
Mtandao huo wa mawasiliano
unatoa fursa kwa watoto na au watu wazima kwa niaba ya watoto kutoa
taarifa za ukatili unaofanywa kwa watoto katika eneo fulani ili
kuwezesha wahusika kufuatilia kwa karibu na kutoa msaada kwa
mtoto/watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili kwa kuwachukulia hatua
wahusika wa vitendo hivyo vya ukatili.
Kupokelewa kwa taarifa ukatili
dhidi ya watoto kumeweza kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali ikiwemo makampuni ya simu kwa kumwezesha mtoa taarifa kupiga
simu hiyo bure, Polisi kwenda kukamata wahusika na kuwafikisha sehemu
husika kulingana na Sheria na taratibu za nchi, na hospitali kutoa
huduma kwa wahusika wa matatizo mbalimbali yanayohitaji huduma za
kiafya.
Kuhusu uelewa wa wananchi juu ya
matumizi ya simu 116 (Child helpline), kuripoti taarifa za ukatili kwa
watoto katika maeneo yao, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Mtoto,
anasema wananchi wa Wilaya zile sita zilizo kwenye mradi wa majaribio
(Wilaya/ Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu
na Hai) wameonyesha uelewa wa kutosha na wamekua watumiaji wazuri tu
wa namba hiyo. Hali hii imepunguza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
katika maeneo yao.
Anataja sehemu ambazo kumekua na
changamoto ya matumizi ya simu katika Wilaya hizo teule kuwa ni hasa
zile sehemu za ndani zaidi ama vijijini na kusema bado kupitia wadau
mbalimbali wameweza kusaidia watoto wanaokutwa na ukatili dhidi yao.
“Kumekuwa na uelimishwaji hadi
ngazi ya kata na mtaa juu ya kuripoti taarifa za ukatili dhidi ya
watoto pamoja na ushirikiano wa kazi wa karibu kati yao na maafisa
maendeleo ya jamii na wadau wengine wakiwemo Wanasheria, Maafisa Ustawi
wa Jamii, Halmashauri za Wilaya pamoja na Taasisi za Elimu.”Anasema
Missari.
Mpango wa kuripoti taarifa za
ukatili dhidi ya watoto umekuwa na mafanikio mengi ikiwemo, kusaidia
watuhumiwa wa watoto waliopata madhara mbalimbali kutokana na ukatili
dhidi yao kufikishwa katika vyombo vya sheria mfano wa kesi ya hivi
karibuni ya mtuhumiwa aliyembaka mtoto alihukumiwa kwenda kifungo cha
miaka 30 gerezani na mtoto aliyetoroshwa toka Musoma kuweza kurudishwa
kwa wazazi wake.
Bwana Missari anasema “mfano
tulipata taarifa kutoka kwa jirani kuwa mtoto Nasra ameafanyiwa ukatili
kwa kuwekwa ndani ya boksi kwa muda wa miaka minne huko mkoani Morogoro.
Taarifa hizo tulizifanyiakazi na kufanikiwa kumpeleka mtoto kutibiwa
katika hospitali ya Taifa Muhimbili. Bahati mbaya mtoto Nasra alifariki
dunia Juni mosi mwaka 2014.”
Mtoto Shabani Abdalah mwenye umri
wa miaka 12 anayesoma darasa la tano katika shule ya Msingi Temeke
katika Manispaa ya Temeke jijini Dar salaam ameeleza namna alivyosaidiwa
na matumizi ya namba 116.
“Kwa vile nilisikia shuleni
kuhusu namba 116, niliamua kupiga simu na kuwaeleza namna ambavyo mlezi
wangu ananitesa kwa kunifanyisha kazi ngumu, kuninyima chakula na
kunipiga mara kwa mara, nafurahi kwani nilipata msaada na aliacha
kunifanyia vitendo hivyo”
Pamoja na hayo, fanikio kubwa
kabisa la matumizi ya namba 116 katika kuripoti taarifa za ukatili dhidi
ya watoto ni kuanzishwa kwa ‘One Stop Centre’ iliyopo katika hospitali
ya Amana wilaya ya Ilala mahali ambapo mtoto aliyefikwa na tatizo la
ukatili hukuta huduma zote mahali pamoja kwa maana ya polisi,
mwanasheria, daktari pamoja maafisa maendeleo ya mtoto.
Pia, kumekuwapo na mafunzo
kuhusiana na sheria za mtoto na namna ya kulinda mtoto ikiwa ni sambamba
na kuanzishwa kwa dawati la mtoto katika vituo vya polisi sehemu
mbalimbali nchini.
Pamoja na mafanikio, Mkurugenzi
Msaidizi Maendeleo ya Mtoto Missari anasema kwamba baadhi ya changamoto
zilizojitokeza katika kuendesha mtandao huu ni pamoja na kupokea simu
kutoka karibia mikoa yote ya nchi tofauti na matarajio na maandalizi
yetu ya kupokea simu kutoka kwenye wilaya ambazo zina mfumo wa ulinzi na
usalama wa mtoto.
Tatizo la baadhi ya wilaya na
Kata kutokuwa na maafisa ustawi wa jamii au mfumo wa ulinzi na usalama
wa mtoto. Hili swala linatusababisha kupata kigugumizi pale ambapo
unahitaji kufanya rufaa ya kesi kwa maafisa ustawi wa jamii kwa msaada
zaidi, kwani kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009, maafisa ustawi
wa jamii ndio wanajukumu la kuhakikisha usalama na ustawi mzuri wa
mtoto na kuhakikisha watoto wote wanaishi katika mazingira rafiki na
salama.
Changamoto nyingine ni uhaba wa
wafanyakazi wa kupokea simu hizo hasa wakati wa usiku lakini pia
kukosekana ‘call centre’ za kutosha kuhudumia nchi nzima pamoja na
uelewa mdogo wa wananchi dhidi ya mtandao.
Uanzishaji wa Mtandao wa
Mawasiliano wa Kusaidia Watoto ni mojawapo ya utekelezaji wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Haki za Watoto (The UN Convention on the Rights of
the Child – UN CRC) ambao Tanzania iliusaini na kuuridhia mara baada ya
kupitishwa kwake.
Kwa kiasi kikubwa kama mtandao
utatumiwa kwa malengo haya, ni imani yangu kuwa itasaidia kupunguza
ukatili dhidi ya watoto na vile vile kuhakikisha kuwa watoto wanapata
msaada stahiki na kwa wakati.
Kwa bahati mbaya watoto kama
Ndyimiake Kiswigo mwenye umri wa miaka tisa anayesoma darasa la pili na
Subilaga Kiswigo mwenye umri wa miaka nane anayesoma darasa la kwanza
wote katika shule ya Msingi Chemuchemu katika Manispaa ya Iringa mjini,
mkoani Iringa wanasema hawajui chochote kuhusu namba 116, licha ya kuwa
wanasikia watoto wenzao wakifanyiwa vitendo vya ukatili katika mazingira
yao.
Pia, mtu kama Avelina Mushi
mwenye umri wa miaka 60, mkazi wa Kibosho Kirima mkoa wa Kilimanajro,
wilaya ya Moshi vijijini, anasema hawajawahi kusikia namba 116 kuhusu
kutoa msaada kwa watoto, lakini anaipongeza Serikali kwa juhudi hizi za
kutafutia ufumbuzi tatizo la ukaliti na unyanyasaji kwa watoto, huku
akiitaka itoe elimu kwa wananchi wengi kuhusu matumizi ya namba hiyo ili
waweze kuwaokoa watoto katika matatizo mbalimbali.
Child Helpline International
(CHI) ni Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na uanzishaji wa
mitandao ya mawasiliano ya kusaidia watoto. Tanzania ni moja ya nchi
zinazotumia mitandao yenye kuhudumia watoto zikiwemo Afrika ya kusini,
Kenya na Swaziland
0 comments:
Post a Comment