Home » » BARRICK YADAIWA KUWANYANYASA WAFANYAKAZI WAKE

BARRICK YADAIWA KUWANYANYASA WAFANYAKAZI WAKE

na Betty Kangonga
MENEJIMENTI ya Kampuni ya Barrick Gold Mining ambao wanaendesha mgodi wa Bulyanhulu, imetupiwa lawama ikidaiwa kupindisha sheria za nchi na kuwafukuza wafanyakazi kinyume na utaratibu.
Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo ambao walifika jijini Dar es Salaam ili kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walijikuta wakiachishwa kazi mwaka 2007 baada ya kugundulika kupata ugonjwa wakiwa kazini.
Wakizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wafanyakazi watatu wa kampuni hiyo, walisema kuwa menejimenti imekuwa ikitumia kigezo cha ugonjwa, na kupeleka majina katika Bodi ya Tiba na kisha kuwaachisha kazi.
Wafanyakazi hao ambao wanakabiliwa na maumivu makali ya magonjwa yaliyotokana na kazi walizokuwa wakizifanya, walisema kuwa Barrick hutumia nafasi hiyo ili kukwepa kulipa fidia inayohitajika kimataifa.
Baadhi ya wagonjwa hao wanahitajika kufanyiwa upasuaji, na mmoja anatakiwa kupelekwa nje ya nchi kutokana na kukosekana wataalamu nchini, lakini wameendelea kutaabika pasipo kuelewa hatima yao.
Mmoja wa wagonjwa hao ambaye amepangiwa chumba katika Hoteli ya Durban, Khalfan Lukensa, alisema kuwa alipata matatizo ya kuziba kwa njia ya hewa pamoja na kuvuja damu sehemu za siri baada ya uti wa mgongo kuathirika kutokana na kuendesha mashine nzito.
“Unajua nilianza kusikia matatizo ya kiafya mwaka 2006, lakini ilipofika 2009 yalizidi, nilikuwa naendesha moja ya mashine iitwayo Scoop,” alisema.
Alisema daktari wa kampuni aliamua kumwandikia rufaa na kuja Muhimbili na baada ya vipimo aligundulika kuwa aliathirika katika mfumo wa hewa na uti wa mgongo, hivyo kutakiwa kupelekwa nchini India katika Hospitali ya Bangalore kwa ajili ya upasuaji.
Alisema cha kustaajabu, alibaini taarifa za kopi ya ripoti yake kuibwa na kubadilishwa, ikawapo iliyoonesha kuwa tatizo lake alilipata tangu awali akiwa hajaajiriwa katika kampuni hiyo.
“Walifanya hivyo ili kukwepa gharama, maana ninatakiwa kulipwa hisa tano na kunitunza hadi kifo, kwani kuna mfano wa mzungu mmoja (anamtaja) alipata tatizo kama langu, hadi sasa analipwa na kutunzwa, na walimgharamia tangu yupo hapa hadi aliporudi kwao,” alisema.
Alisema kuwa hadi sasa hajui hatima yake, na madaktari walimweleza kuwa iwapo upasuaji hautafanyika kwa haraka, kuna hatari ya kupooza mwili wake.
Lukensa, alisema kuwa baada ya kuvutana sasa wamempa hifadhi katika Hoteli ya Durban na kumlipia gharama za mazoezi, lakini hana mtu wa kumwangalia maana kuna wakati hali yake inakuwa mbaya.
Kwa upande wao, Haji Luge na Bakari Ally walisema wamekuwa wakiishi kwenye Hoteli ya Durban jijini Dar es Salaam kwa miaka miwili sasa, huku wakiugua maradhi waliyopata kutokana na kazi ya mgodini.
Luge alishafanyiwa operesheni ya tumbo mara mbili, baada ya kupata ajali mgodini, na sasa anasubiri operesheni nyingine inayogharimu sh milioni mbili.
Naye Ally alisema ana matatizo ya kifua na kiuno, ambayo ameyapata kazini. Sasa anasubiri kufanyiwa operesheni ya kwanza.
Alisimulia kwamba mwaka 2007, walikuwa miongoni mwa wafanyakazi wapatao 1,000 waliofukuzwa Barrick baada ya kutokea mgogoro wa kimaslahi, uliosababisha mgomo, lakini baadae ilibainika majina yao yalijumuishwa kimakosa, kwa sababu wakati wa mgogoro huo walikuwa kwenye matibabu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus Mgaya, alikiri kuwafahamu watumishi hao, na kwamba suala hilo aliliwasilisha serikalini ambako waliahidi kulishughulikia.
Msemaji wa Barrick, Nestor Foya, alipoulizwa juu ya madai hayo, alisema kuwa wanamtambua Lukensa na kusema kuwa ni mfanyakazi wao, na kwa sasa anatibiwa kupitia kadi ya matibabu ya AAR.
Alisema kuwa taarifa ya daktari wake haijaeleza iwapo ugonjwa unaomkabili unatakiwa kupelekwa India, hivyo alimshauri iwapo anahitaji kupata msaada kupitia kampuni, aandike barua na kuomba kuliko kupeleka taarifa katika maeneo yasiyotakiwa.
Kuhusu kutumia Bodi ya Tiba kufukuza wafanyakazi, alisema kuwa kampuni hiyo haina suala hilo kwa kuwa bodi hiyo uundwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, na kwamba wao wana Bodi ya Afya Kazini (Occupational Health Reveal Board) ambayo haijihusishi na suala lolote la kufukuza wafanyakazi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa