Home » » DC GEITA AZIMA MKAKATI WA DAKTARI KUFUKUZWA

DC GEITA AZIMA MKAKATI WA DAKTARI KUFUKUZWA

Na Victor Bariety, Geita
MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale, Ibrahimu Marwa, amekataa hoja zilizotolewa na baadhi ya madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka daktari wa mifugo kutimuliwa kwa madai ya kufunga minada yote ya mifugo na kuwataka waheshimu kazi zinazofanywa na wataalamu na si kuzichanganya na siasa.

Daktari huyo, Thobias Kiputa, alifunga minada hiyo inayodaiwa kuwa chini ya zabuni ya baadhi ya madiwani na watendaji wa umma baada ya ugonjwa wa miguu na midomo ulioibuka mwanzoni mwa Mei, mwaka huu wilayani Geita na Nyang’hwale na kuthibitishwa na Kituo cha Uchunguzi wa Maradhi ya Mifugo Kanda ya Ziwa (VIC).

Kutokana na hali hiyo, madiwani hao walimtaka DC Marawa kuagiza minada hiyo kufunguliwa mara moja, ikiwa ni pamoja na kumwajibisha daktari huyo kwa walichodai hakutenda haki, hasa ikizingatiwa kuwa wakazi wa maeneo hayo wanategemea kuendesha maisha yao kwa kuuza mifugo.

Hoja ya kutaka daktari huyo awajibishwe ilianzishwa na Diwani wa Nyijundu (CCM), Jackob Nyanda, aliyetaka awajibishwe kabla wao hawajamkataa katika vikao vyao vya baraza, liwe fundisho kwa wataalamu wengine wanaofanya kazi kwa kukurupuka.

“Mkuu hapa Nyang’hwale minada yote ya mifugo imefungwa na daktari wa mifugo kwa maslahi yake binafsi na sasa wananchi wanashindwa kuendesha maisha yao kwa kukosa kipato, maana wengi hutegemea kuuza mifugo, hivyo tunakuomba kabla sisi madiwani hatujamkataa, uagize afungue minada na umwajibishe mara moja.

“Miaka yote hatujawahi kusikia mifugo inaugua na sisi ndiyo wafugaji wakuu, sijui huyu daktari anatutaka nini sisi wana Nyang’hwale, hakika ametukwaza na wewe kama Serikali tunaomba hilo ulifanyie kazi mara moja,” alisema Nyanda.

Kwa upande wake, Diwani wa Kharumwa, Marco Masusu, alisema: “Jamani madiwani wenzangu mimi naona mnampa mzigo mkubwa mkuu wetu wa wilaya wakati hilo ni jukumu letu sisi, tunasubiri katika vikao vyetu vya baraza tutamfukuzilia mbali huyu daktari, tena suala hilo mniachie mimi, hatuwezi kubabaishwa na mtu mdogo kama daktari wakati sisi ndiyo tumeshika mpini.”

Hata hivyo, DC Marwa aligeuka mbogo ambapo mbali na kupinga hoja hiyo, aliwataka madiwani hao kutochanganya siasa na kazi za kitaalamu iwapo wanataka kuwaletea wananchi maendeleo.

“Ndugu zangu nimewasikia na wote madiwani karibu watano mliosimama mmezungumzia kuhusu daktari kufunga minada na mnataka Serikali imwajibishe kabla ninyi hamjamkataa katika vikao vyenu.

“Ninachotaka kuwaeleza ni kwamba nchi hii haiendeshwi hivyo na kama siasa itapenyeza hadi katika masuala ya kitaalamu hatutafika ndugu zangu, ninachojua mimi daktari amefunga minada kutokana na ugonjwa ulioibuka na si uongo, ugonjwa huo upo na umethibitishwa na VIC, sasa nyie mnaposema hakuna ugonjwa nani kawaeleza hilo.

“Ifike mahala siasa ibaki kuwa siasa na masuala ya kitaalamu waachiwe wataalamu, vinginevyo mtafukuza kila mtu mnayetaka afanye kazi kisiasa na kuacha kutekeleza majukumu yake kama taaluma yake inavyomuelekeza na kwa hilo mimi siwezi kuunga mkono, ila nitakachokifanya ni kuhakikisha chanjo ya mifugo inafanyika haraka ili minada ifunguliwe,” alisema Marwa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa