na Victor Eliud, Geita
MKUU wa Wilaya (DC) ya Nyang’hwale, Ibrahimu Marwa, amezikataa hoja za madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotaka daktari wa mifugo wa wilaya hiyo, atimuliwe kwa madai ya kufunga minada yote ya mifugo.
Daktari huyo, Thobias Kiputa, alifunga minada hiyo inayodaiwa kuwa chini ya uzabuni wa baadhi ya madiwani na watendaji wa umma, baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa miguu na midomo mwanzoni mwa Mei mwaka huu, wilayani Geita na Nyang’hwale.
Kufuatia hali hiyo, madiwani hao walimtaka mkuu huyo wa wilaya kuagiza minada hiyo kufunguliwa mara moja, ikiwa ni pamoja na kumwajibisha daktari huyo kwa walichodai hakutenda haki, hasa ikizingatia kuwa wakazi wa maeneo hayo wanategemea kuendesha maisha yao kwa kuuza mifugo.
Hoja ya kutaka daktari huyo aondolewe kwenye wilaya hiyo ilianzishwa na Diwani wa Kata ya Nyijundu, Jacob Nyanda, ambaye alimtaka mkuu huyo wa wilaya kumwajibisha kabla wao hawajamkataa kwenye vikao vyao.
“Mkuu hapa Nyang’hwale minada yote ya mifugo imefungwa na daktari wa mifugo kwa masilahi yake binafsi, na sasa wananchi wanashindwa kuendesha maisha yao kwa kukosa kipato, maana wengi hutegemea kuuza mifugo, hivyo tunakuomba kabla sisi hatujamkataa, uagize afungue minada na umwajibishe mara moja,” alisema na kuungwa mkono na wenzake.
Hata hivyo katika hali ambayo hawakuitegemea, baada ya kusimama kujibu hoja zao, mkuu huyo aligeuka mbogo ambapo mbali na kuwapinga, aliwataka madiwani hao kutochanganya siasa na kazi za kitaalamu iwapo wanataka kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ndugu zangu nimewasikia na wote madiwani karibu watano mliosimama mmezungumzia kuhusu daktari kufunga minada na mnataka serikali imwajibishe. Ninachotaka kuwaeleza ni kwamba nchi hii haiendeshwi hivyo,” alisema.
Alisema ifike mahala siasa ibaki kuwa siasa na masuala ya kitaalamu waachiwe watalaamu, vinginevyo watamfukuza kila mtu wanayetaka afanye kazi kisiasa na kuacha kutekeleza majukumu yake kama taaluma yake inavyomwelekeza.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akizungumza na watendaji wa kata na vijiji, madiwani pamoja na viongozi wa dini katika wilaya hiyo kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuijenga wilaya hiyo mpya ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment