na Ali Lityawi, Geita
MTOTO, Ernest Thomas (15), mkazi wa Kijiji cha Msasa, Tarafa ya Busanda wilayani Geita, leo anatarajiwa kukatwa mguu uliopata kiupele na kuoza akiwa na mwaka mmoja, baada ya Mfuko wa Victoria Foundation kufanikisha matibabu yake.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambako ndiko yalikofanyikia matibabu ya mtoto huyo, Profesa William Mahalu, alisema wamelazimika kumfanyia matibabu ya kuukata mguu kutokana na kukabiliwa na ugonjwa wa saratani ya mfupa uliosababisha kuoza kwa mguu huo.
Akiongea na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa Mfuko wa Victoria Foundation,Vicky Kamata, alisema alibaini matatizo ya mtoto huyo wakati alipokuwa kwenye shughuli za kibunge katika Kijiji cha Msasa ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake.
Kamata alisema alielezwa na wazazi wa mtoto huyo kuwa maradhi hayo mtoto wao aliyapata tokea akiwa na mwaka mmoja, lakini kutokana na kipato duni jitihada za kumtibu zilishindikana.
Kamata alisema kuwa kutokana na mfuko wake kujihusisha zaidi na masuala ya kijamii aliamua kumchukua yeye na mwenziwe Jeremiah Julius (13) mkazi wa Kijiji cha Numve, Tarafa ya Butundwe wilayani Geita ambaye naye kwa mujibu wa madaktari alikuwa akikabiliwa na saratani ya mfupa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
“Mguu wa Julius unatarajiwa kukatwa leo katika Hospitali ya Bugando ambapo wote pamoja na Timothy aliyekatwa juzi wamelazwa,” alisema Kamata.
Akielezea sababu za chanzo cha ugonjwa huo mzazi wa Ernest, Thimothy Chunguye, alisema mtoto wake alianzia kuvimba upele, baada ya kuukuna ulianza kidonda ambacho baadaye kilienea mguu wote na kuufanya uoze na kutoa harufu mbaya iliyodumu kwa miaka kumi na tano hadi juzi ulipokatwa kwa ufadhili wa Victoria Foundation.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment