Home » » WAANDISHI WAZUIWA HALMASHAURI GEITA

WAANDISHI WAZUIWA HALMASHAURI GEITA

 Na Victor Bariety, Geita
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita, Tatala Mpangalukela, jana alizuia waandishi wa habari kuingia katika kikao cha Baraza la Madiwani, lililokuwa likijadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hatua hiyo ilibainika baada ya Ofisa Utumishi wa wilaya hiyo, Charles Kimaro na Mweka Hazina, Victor Swai, kujifanya mabaunsa mlangoni kuhakikisha waandishi wa habari hawaingii ukumbini humo.

Kutokana na hali hiyo madiwani waligeuka mbogo na kuhoji sababu za kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye kikao hicho, kilichokuwa kinajadili taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha 2010/11.

Hali hiyo ilisababisha madiwani kuvutana na Mkurugenzi, baada ya kuhoji sheria iliyotumika kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye kikao hicho, ilhali kilikuwa cha wazi kujadili utendaji na utekelezaji wa maendeleo kupitia hoja zilizowasilishwa na CAG.

Hatua hiyo ilisababisha madiwani kutumia muda wa dakika 15 kujadili suala hilo, hadi Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, alipoingilia kati na kumtaka mkurugenzi kuwaruhusu kuingia kwenye kikao hicho mara moja.

"Mkurugenzi kwa nini umewazuia waandishi wa habari kuingia kwenye kikao hiki, kwani kuna siri gani humu? Naomba waingie mara moja...waiteni haraka sana,’’ alisema Magalula.

Awali Mwenyekiti wa Kabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita, Victor Bariety, alituma ujumbe kwa njia ya simu kwenda kwa mkuu wa mkoa akitaka ufafanuzi kuhusu kufukuzwa kwa waandishi hao.

Awali akijibu hoja ya kuzuiliwa kwa waandishi wa habari katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Christopher Kadeo, alitaka ufafanuzi kutoka kwa Tatala sababu za kuzuiliwa kwao.

RC Magalula alishangazwa na hatua hiyo na kumtaka mkurugenzi kuhakikisha waandishi wa habari wanarudi kwenye kikao hicho, huku akionya kitendo kama hicho kisijirudie tena kwenye halmashauri zote katika mkoa wa Geita.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa