Home » » Mgonjwa adai fidia ya Mil.30 baada ya kung'olewa meno matatu kimakosa

Mgonjwa adai fidia ya Mil.30 baada ya kung'olewa meno matatu kimakosa



Na David Azaria, Geita-Geita Yetu 
Zahanati ya kata ya Nkome wilayani Geita mkoani Geita imeingia kwenye kashfa kubwa kufuatia Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo Gamba Gamba kumng’oa meno mazima matatu badala ya jino moja lililokuwa likimsumbua mgonjwa aliyefika kwenye zahanati hiyo Rejina Lucas (30) mkazi wa kijiji cha Nkome. 
  
Kufuatia kitendo hicho kinachodaiwa kwenda  kinyume na huduma aliyokuwa akihitaji mgonjwa huyo,Baba mzazi wa binti huyo Lucas Paul ametoa siku saba kwa mganga mfawidhi wa zahanati hiyo awe ametoa fidia kwa hasara ya uharibifu wa meno ya binti yake. 
  
Akizungumza na Waandishi wa habari Paul alisema tayari amemuandikia barua mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo na kumpa hizo siku saba awe ametoa fidia kwa kuwa ameenda kinyume na maadili ya kazi yake na kumsababishia Rejina kuwa kibogoyo. 
  
Paul alifika kwenye zahanati hiyo Juni 16 mwaka huu akiwa na binti yake huyo aliyekuwa anasumbuliwa na jino moja ambalo alihitaji ling’olewe lakini badala ya kung’olewa jino moja aling’olewa meno matatu kwa malipo ya shilingi 30,000/=. 
  
kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na baba mzazi kwenda kwa mganga huyo na nakala kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Benson Tatala,Mganga mkuu wa wilaya Omar Dihenga,ofisi ya Takukuru wilaya na mkuu wa kituo cha polisi Geita,amekusudia kumfungulia shauri la mashtaka  mahakamani kama hatalipa fidia ndani ya siku saba. 
  
 “Kutokana na madhara ambayo ameyapata Rejina na wewe kukiuka miiko ya kazi umesababisha binti yangu awe kibogoyo ameanza kupukutika meno zaidi ya lile moja ulilolazimisha kuling’oa tena kwa thamani ya shilingi 30,000/= wakati ni kinyume kabisa na maadili ya kazi yako”ilisema sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa juni 17 mwaka huu. 
  
Mzazi huyo anahitaji kulipwa Fidia ya Sh.30, 000, 0000 kutokana na maumivu na uharibifu aliofanyiwa mwanaye, huku akisistiza kwamba endapo Mganga huyo hatafanya hivyo kwa wakati unaotakiwa atakwenda kudai haki hiyo mahakamani. 
  
Tukio kama hili liliwahi kutokea miaka kadhaa iliyopita huko jijini Dar es Salaam ambapo badala ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji kwenye Goti alifanyiwa kichwani, ingawa hili la Geita Mgonjwa amefanyiwa mahali palipotakiwa ingawa si kwenye kiini penyewe. 
  
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Geita Dk Ndalo Ndalo alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa wamemuita mganga huyo na kumtaka atoe maelezo kuhusiana na tukio hilo. 
“Baada ya kupata taarifa hizi kupitia nakala ya barrua hii kamamnavyoiona….tumeamua kumuita mganga wetu kwa ajili ya kujua ukweli,amekiri kufanya jambo hili,kwa hiyo hatua ya awali tulioichukua kwa sasa ni kumtaka kutoa maelezo kwa njia ya barua ili tujue pa kuanzia……’’ alisema Dk.Ndalo. 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa