Na David Azaria, Geita-Geita Yetu
SIKU chache baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kumkaribisha kwa kishindo Kamanda Mpya wa polisi Mkoani Geita Leonard Paul kwa kutaka kumuua Mkuu wake wa kituo, Kamanda huyo naye amejibu mapigo kwa kishindo baada ya kumuua jambazi mmoja na kuwakamata wengine watatu.
Majambazi hao wanaodaiwa kufanya shambulizi la kutaka kumuua aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Katoro Thomas Mboya kwenye Baa Mkoani Geita, wametiwa mbaroni na Polisi huku Mmoja akiuuawa kwa kupigwa Risasi baada ya kumrukia polisi kwa lengo la kutaka kumpora silaha.
Watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika mji Mdogo wa Buselesele wilayani Chato Mji ulioko mpakani kati ya wilaya za Geita na Chato umbali wa mita 100 kutoka katika Mji wa Katoro ambapo walifanya shambulio la kutaka kumuua Mkuu wa Kituo cha Katoro.
Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Leonard Paul alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kumtaja aliyeuawa kuwa ni Leonard Nana (30)Mkazi wa Mji Mdogo wa Katoro,ambaye hata hivyo urai wake bado unaleta utata baada ya kukutwa akiwa na Paspoti ya Nchini Burundi.
Kamanda Paul alisema siku ya tukio polisi wa kituo kidogo cha Buselesele wilayani Chato walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba watuhumiwa hao waliokuwa katika Nyumba ya kulala wageni ya Nyamigogo walikuwa wakipanga njama za kwenda kufanya uhalifu.
“Baadhi ya raia wema waliopata kusikia mazungumzo ya watuhumiwa hao waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Buselesele ambao baadaye walifanya mawasiliano na wenzao wa kituo kidogo cha Katoro kwa kuwa viko karibu,ambapo jumla ya askari watano wakiwa na silaha walifika katika eneo hilo……’’ alisema Kamanda Paul nakuongeza.
“Walipofika walifanikiwa kuwakuta watuhumiwa ambao kwa wakati huo hawakuwa na silaha ya aina yoyote ambapo waliwaweka chini ya ulinzi na kuwakamata,hata hivyo mmoja wa watuhumiwa hao(Marehemu),aliamua kupamba na mmoja wa maaskari polisi kwa lengo la kumpora Bunduki hali iliyosababisha apigwe risasi kwenye mguu wa kushoto…….’’.
Alisema watuhumiwa hao walichukuliwa hadi kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Geita na kuwekwa ndani huku majeruhiwa aliyepigwa risasi akikimbizwa hospitali ya wilaya kwa matibabu, lakini alifariki Dunia baadaye.
Baada ya kuhojiwa na kupekuliwa iligundulika kuwa watuhumiwa hao ni raia kutoka nchini Burundi ambao aliwataja kwa majina ya Nsengiyumvua Elira (25),Eliye Habyarimana (28) wote wakazi wa Mkoa wa Ruyigi nchini Burundi,pamoja na Mabula Lawrent ((29) mkazi wa kijiji cha Runzewe wilayani Bukombe Mkoani Geita.
Hata hivyo Kamanda Paul ameonekasna kushangazwa na ujasiri wa watuhumiwa hao wa kuendelea kuwepo katika eneo la tukio walilotaka kumuua askari polisi huku wakijua kwa dhati kwamba wanatafutwa na polisi kwa lengo la kukamatwa,na kibaya zaidi wakipanga njama za kufanya uhalifu mwingine katika eno hilo hilo!.
“Watu wa huku wanaonekana ni wakatili sana,hawa watu wamefanya uhalifu hapahapa katoro,wamejeruhi watu na almanusra wamuue mkuu wa kituo cha polisi katoro,walijua kabisa kwamba tunawatafuta lakini bado wakaendelea kuwepo kwenye eneo hilo,na kibaya zaidi wakawa wanapanga mikakati ya uhalifu……….hii ni roho ya ukatili ambayo sisi jeshi la polisi hatuwezi kuivumilia…..’’ alifafanua Kamanda Paul.
Aliwapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kutoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kusisitiza kwamba Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Geita liko makini na Imara katikia kuhakikisha kwamba linapambana na kila mtu ambaye ana mawazo hasi ya kufanya uhalifu.
“Labda kwanza niwapongeze wananchi wa mkoa huu kwa sababu wameonekana kutupa ushirikiano wa karibu sana na huu ni utekelezaji wa wito wangu ambao nimekuwa nikutoa mara kwa mara kwao,lakini pili niseme tu kwamba niliahidi kwamba jeshi la polisi litatumia kila mbinu kuhakikisha kwamba watuhumiwa hawa wanakamatwa hilo limetekelezwa,ingawa Bunduki bado lakini nazo ziko mbioni tutazipata tu,hiyo ni lazima na wala si ombi maadam tunao mikononi mwetu,bahati mbaya tu huyo mmoja kafariki…..’’ aliongeza.
Wiki iliyopita watuhumiwa hao walimvamia aliyekuwa Mkuu wa kituo cha Polisi Katoro Inspekta Mboya wakati akiwa Baa kwa lengo la kumuua kwa bunduki,lakini hata hivyo alifanikiwa kupambana nao kabla hawajmfyatulia risasi na kufanikiwa kuwatoroka na kukimbia,tayari jeshi hilo limechukua hatua za kumhamisha Mkuu huyo wa Kituo na nafasi yake kuchukuliwa na mwingine.
0 comments:
Post a Comment