Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Jovina Bujulu-MAELEZO
USAMBAZAJI
wa nishati ya umeme unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
umewezesha Wananchi wengi walioko vijijini kuanzisha miradi mbalimbali
ya kiuchumi na kijamii.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa REA nchini Dkt. Lutengano Mwakahesya,
nishati bora inachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa jambo ambalo
linasaidia kuboresha hali ya maisha ya Wananchi wengi walio vijijini.
Kwa kutambua umuhimu huo REA kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali
imeweza kuibua miradi mbalimbali ya nishati vijijini ili Wananchi waweze
kufaidika nayo.
Wadau
hao ni pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti
wa Bei za Bidhaa (EWURA), Wizara ya Nishati na Madini, Asasi zisizo za
Kiserikali (AZISE), Asasi za Kijamii (AZAKI) na Sekta binafsi. Dkt.
Mwakahesya ameainisha miradi ya nishati za umeme kuwa ni pamoja na zile
zinazotumia nguvu ya upepo, jua, maji na bayogasi.
Dkt. Lutengano ameeleza kwamba, lengo kubwa la ushirikiano baina ya REA na Wadau hao ni kuibua miradi mbalimbali ya nishati, kutoa
ruzuku na kuwezesha upatikanaji wa ushauri wa kitaaluma kwa
waendelezaji wenye sifa katika masuala ya kiufundi, usimamiaji,
uchanganuzi wa kifedha, ugharamiaji wa miradi na mienendo mizuri ya miradi hiyo.
Amesema,
REA inahakikisha kwamba uendelezaji wa miradi ya nishati vijijini
unazingatia utumiaji wa mazingira ili kutunza vyanzo vingine vya
nishati. Ameongeza kusema kuwa REA inaongozwa na Bodi ya Nishati
vijijini ambayo husimamia uendeshaji wa Mfuko wa Nishati vijijini (REF).
Mfuko huu unasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa miradi ya Nishati.
Serikali
kupitia mfuko wa Nishati vijijini ilifadhili miradi kabambe ya
usambazaji wa umeme vijijini awamu ya kwanza na ya pili ambayo
inatekelezwa na Wakandarasi binafsi katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Utekelezaji
wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 90 na ambapo kilometa 1600 za
msongo wa kati na kilometa 97 za msongo mdogo zimejengwa na vipoza umeme
vilifungwa na wateja wa awali 18,253 wameunganishiwa umeme.
Katika
awamu ya pili mradi ulilenga kujenga vituo 6 vya kuongeza msongo wa
(umeme 11/33 KV) katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga
na Tunduru, ujenzi wa njia za umeme msongo mdogo na wa kati na kufunga
mashine umba (transfomer) 3100. Mradi ulilenga kuunganisha wateja
225,000 na vijiji 2,500 pindi ukikamlika na kupeleka umeme makao makuu ya Wilaya 13.
Mradi
huu uliweza kujenga vituo 6 vya kuongeza nguvu Kigoma Vijijini, Kasulu,
Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru.Aidha mradi ulikamilisha ujenzi wa
njia za msongo mdogo na wa kati,na wateja 61,023 walipatiwa umeme. Jumla
ya vijiji 1,162 viliunganishwa kwenye gridi.
Akielezea juu ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizoanzishwa vijijini Dkt. Lutengano amesema, kutokana na upatikanaji wa
nishati ya umeme vijijini maisha ya Wananchi yamekuwa mazuri kutokana
na kuwepo kwa shughuli za kibiashara kama vile, mashine za kusaga na
kukoboa nafaka, viwanda vya uselemala, utengenezaji wa milango na
madirisha ya chuma, uuzaji wa vinywaji baridi n.k.
Kwa
upaande wa shuhguli za kijamii, upatikanaji wa nishati wa umeme
umeboresha huduma za hospitali, vituo vya afya na kumeongezeka kwa ari
ya wanafunzi kujisomea wakati wote na pia matumizi ya kompyuta
mashuleni, Kwa sasa wanawake wajawazito wanakwenda hoapitalini
kujifungua bila kulazimika kuchukua koroboi.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, hadi
mwaka 2014 kiwango cha uunganishaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya
na vijijini ulifikia asilimia 24 na kufanya Wananchi wanaopata huduma za
umeme kufikia asilimia 36 ya Watanzania waishio bara ukilinganisha na mwaka 2005 ambapo kiwango cha uunganishaji umeme kilikuwa chini ya asilimia 10.
Raarifa
hiyo inaonesha kwamba ongezeko hilo linatokana na juhudi mbalimbali za
Serikali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati vijijini
(REA) na kupunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja na
kuhamasisha Wananchi kutumia umeme.
Jumla ya shule za sekondari 1845, zahanati na vituo vya afya 898 na
hospitali 96 zimepatiwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali
nchini. Aidha, Wakala kwa kushirikiana na TAZAMA pipeline na Mfuko wa
Maendeleo wa Mafia umewezesha utekelezaji wa miradi miwili ya kupeleka
umeme katika pampu za kusukuma maji na mafuta za TAZAMA zilizoko Kisanga
(Morogoro).
Akizungumzia
mafunzo yanayofadhiliwa na Wakala kwa wananchi, Meneja wa Tathmini na
Ufuatiliaji wa REA , ndugu Vestina Rwelengera alisema kwamba ni pamoja
na kuwapatia mafunzo yote ya nishati, mfano utunzaji wa vyakula kwa kutumia nishati ya jua, miradi ya umwagiliaji, kukausha samaki na mboga mboga.
Alitaja maeneo yaliyonufaika na na
mafunzo hayo kuwa ni Bagamoyo, Mafia na Somanga Fungu ambapo wananchi
walipata mafunzo ya kutengeneza mkaa kwa kutumia majani makavu. Pia Wakala
kupitia mfuko wa Nishati Vijijini, ulitoa ruzuku kwa vikundi
vinavyotayarisha maandiko ya miradi ili kuwawezesha wanavijiji kupata
mikopo kutoka kwenye benki zilizokubaliana na Mfuko huo.
Akizungumzia
miradi mingine iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ya usambazaji
wa umeme vijijini ndugu Vestina aliema kwamba ni pamoja na mradi wa
SAGCOT Cluster ambao utasambaza umeme kilometa 100 , kujenga kituo cha kupozea umeme katika mji wa Ifakara na mradi huu utaunganisha wateja 3,000.
Miradi
mingine ni ya Andoya ( Mbinga), Tulila (Songea), Yovi (Kilosa), ambayo
imeanza uzalishaji. Miradi ya Maguta ( Kilolo), Lupali (Njombe), na
Isigula (Ludewa) ambayo imeanza kazi ya ujenzi na miradi ya Mwenga
(Mufindi) ambapo jumla ya wateja zaidi ya 4,600 wameunganishwa.
Hadi kufikia Desemba 2015 vijiji 5,009 ambavyo ni sawa na asilimia 33 vilikuwa vimeunganishwa na huduma za umeme na miradi inayoendelea itaunganisha vijiji vingine vipya 1,340 na kufanya jumla ya vijiji 6,349 kupata huduma ya umeme miradi ikikamilika.
Akizungumzia
changamoto zinazoikabili Wakala, ndugu Vestina alisema kuwa ni pamoja
na Wananchi wa vijijini kushindwa kumudu gharama za kuunganishiwa umeme,
upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha na usalama wa miundombinu
kutokana na uharibifu na vitendo vya uharibifu vinavyofanywa na
wananchi.
0 comments:
Post a Comment