Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Wizara
ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi imekanusha kodi ya ng’ombe iliyoripotiwa na
Umoja wa wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao yake wa Wilaya ya Kinondoni.
Taarifa
hii imetolewa na Katibu Mkuu (Mifugo) wa Wizara hiyo Dkt. Mary Mashingo
baada ya kuyaona malalamiko ya wafanyabiashara hao kwenye baadhi ya
vyombo vya habari nchini.
Katika
taarifa hiyo wizara imekanusha kuwa kodi ya ng’ombe siyo shilingi
18,500 kama ilivyoripotiwa na wafanyabiashara hao bali ni shilingi
12,000 ambayo inatambulika kisheria.
“Wizara
yetu inapenda kutoa ufafanuzi juu ya kodi inayotozwa katika machinjio
ya Kimara kama ifuatavyo: ushuru wa soko shilingi 5000, ushuru wa
kusafirisha mifugo shilingi 1500, ushuru wa ukaguzi wa wanyama shilingi
2500 pamoja na gharama za machinjio shilingi 3000 kwa kila kichwa cha ng’ombe ambapo jumla yake ni shilingi 12,000”alisema Dkt.Mashingo.
Aidha,taarifa hiyo
imeelezea kuhusu kupitisha ng’ombe katika soko la upili la Pugu kabla
ya kuwapeleka katika machinjio ya Kimara kuwa ni kwa ajili ya kuwafanyia
vipimo vya afya ng’ombe hao kabla ya kuchinjwa pamoja na kulipia tozo
ya Serikali.
Taarifa
hiyo pia imefafanua baadhi ya sababu za kufungwa kwa machinjio ya
Kimara tangu Aprili 9 mwaka huu zikiwemo za baadhi ya wafanyabiashara
kupeleka ng’ombe katika machinjio hayo moja kwa moja bila kupitia Pugu
ambalo ni kosa kisheria pamoja na uchafu uliokithiri katika machinjio
hayo.
Katika kufanya juhudi za kupambana na matatizo haya,Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi inajipanga kukutana na wafanyabiashara wa
mifugo na mazao yake ili kuwaelimisha zaidi kuhusu Sheria, Kanuni, na
Taratibu zinazopaswa kufuatwa katika ufanyaji wa biashara hii.
0 comments:
Post a Comment