Chato. Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe amemuweka mahabusu mwandishi wa gazeti hili wilayani hapa kwa madai ya kuingia hospitali ya wilaya bila kibali chake.
Mwandishi huyo, Baraka Rwesiga alikamatwa juzi saa 5.04 asubuhi na askari wa Kituo cha Polisi Chato muda mfupi baada ya kufika hospitalini kwa lengo la kuonana na mmoja wa madaktari ili kupata ushauri ya kitabibu.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Latson Mponjoli alisema mwandishi huyo alikamatwa kwa amri ya mkuu wa wilaya.
Mponjoli alisema Mganga Mfawidhi, Dk Lugobert Kalisa alimpigia simu mkuu wa wilaya kumtaarifu kuwa mwandishi huyo alikuwa hospitalini hapo bila kibali, ndipo aliwataarifu polisi ambao walikwenda kumkamata.
Alipotakiwa kuzungumzia amri ya kukamatwa kwa mwandishi huyo, Ntarambe alisema hakuwa na muda, badala yake alimtaka mwandishi wa habari hizi kumtafuta baadaye na hata alipotafutwa hakupatikana.
Akizungumzia suala hilo, Rwesiga alisema alikwenda hospitalini hapo kwa lengo la kuonana na mganga ili kumpa ushauri wa kitabibu kutokana na tatizo la kiafya ambalo limekuwa likimsumbua tangu mwaka 2013.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Kalisa alikiri kukamatwa kwa mwandishi huyo.
Juzi, Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Nape Nnauye alielezea kusikitishwa na matukio ya baadhi ya watendaji serikalini kuwawekea kinyongo waandishi wa habari wanaoripoti udhaifu katika maeneo yao ya kazi, kiasi cha kufikia kuagiza polisi kuwakamata.
CHANZO: MWANANCHI.
CHANZO: MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment