Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imesema itawafukuza kazi maofisa wa Serikali ambao wanaweka
vikwazo na kuwakwamisha waandishi wa habari kushindwa kutekeleza
majukumu yao kwa kupata habari na taarifa mbalimbali kutoka serikalini.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyasema
hayo jijini Mwanza wakati alipozungumza na wadau wa utamaduni, habari na
michezo kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa na
Mwandishi wa Habari wa ITV/ Radio One anayefanyia kazi zake mikoa ya
Kanda ya Ziwa, Cosmas Makongo ambaye alitaka apate msimamo wa Serikali
juu ya hatua zitakazochukuliwa na serikali kutokana na wimbi la
unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali
kwa waandishi wa habari nchini.
Makongo alisema akiwa wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni
alizuiliwa kuandika habari na ofisa mmoja wa Serikali hadi pale
atakapopata kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.
“Kumeibuka wimbi la unyanyasaji wa kijinsia kwa waandishi wa habari,
ukifika Chato huandiki habari mpaka upate kibali kutoka kwa Mkuu wa
Wilaya, nilizuiliwa kuandika habari hivi karibuni wakati nafanya habari
ya uchunguzi wa mabilioni ya fedha wilayani humo,” alisema Makongo na
kuhoji, “Mheshimiwa Waziri tukiendelea kusubiri vibali kutoka kwa
watawala je, tutafichua maovu?” Nape aliongeza kuwa msimamo wa Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni kuvitumia vyombo vya
habari katika kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watu katika
jamii. “Kama kuna Ofisa wa Serikali anaweka kizuizi kwa mwandishi wa
habari ili asipate habari na kushindwa kutimiza wajibu wake tutamfukuza
kazi,” alisema Nape.
Aliwataka maofisa wa habari kote nchini wawe tayari kutoa taarifa
mbalimbali za maendeleo zilizopo kwenye maeneo yao kwa wakati ili
waandishi wauhabarishe umma.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment