Nawakumbuka wapigania haki wa Kiafrika waliowahi kuliongoza ama kulitakia mema bara hili kwa uwezo wao. Watu hawa waliongoza mapambano ya kumfanya Mwafrika awe mtu halisi, wakielewa hatari ilikuwa vipi siku ile mwanakondoo alipokutana na mbwamwitu.
Alipokwenda mtoni kunywa maji, mbwa mwitu
alichanganyikiwa kumwona mwana kondoo mweupe aliyenona akiwa mbele yake.
Alibubujikwa na udenda wa uchu huku akimtafutia staili ya kumla ili
ladha yake isipungue badala ya kuongezeka. Akamwita: “We pumbavu njoo
hapa!” Maskini mwana kondoo asiyejua uadui alimkimbilia, akamwangukia
miguuni na kumwamkia “Shikamoo babu”
Mbwamwitu alifoka: “Watoto wa siku hizi hamna
adabu! Kwa nini unachafua maji hadi mimi mkubwa wako nashindwa
kuyanywa?” Mwana kondoo akajibu, “Babu mimi nilikuwa kule maji
yanakoelekea, wewe upo huku maji yanakotokea.” Staili ya kwanza ikafeli.
Akatafuta ya pili: “Wewe unakumbuka mwaka uleee ulivyonitukana?” Mwana
kondoo akashangaa tena: “Mimi nimezaliwa mwaka huu, hadi sasa nina miezi
minne tu.” Mbwamwitu akaona akifanya mzaha ataukosa mnofu huu.
Akasema: “Basi kama si wewe alikuwa baba yako
maana nilikutana naye hapa hapa!” Mwanakondoo akajibu: “Mama alikuja
hapa kutokea ng’ambo akiwa mjamzito. Mimi sijapata kumfahamu baba
yangu.” Mbwamwitu akasema “Ndiye huyohuyo! Kama si yeye basi ni mama
yako ndiye aliyenitusi maana mmefanana hadi kwato!” Mwana kondoo alizidi
kushangaa, “Mbona mama yangu ni mweusi?” Mbwamwitu kusikia hivyo
alimfuata akiwa tayari kumdhuru: “Si nilisema? Watoto wa kizazi kipya
hamna adabu... Unanitukana tena? Ngoja nikufunde...”
Lakini kwa bahati pale mtoni alikuwapo mbweha
mzee. Akasema: “Unaweza kumla huyo mtoto lakini kamwe hutaijua Elimu
yake. Lakini unaweza kutumia akili zake na ukapata mawindo yako kwa
urahisi. Akili ni bora kuliko mabavu.” Mbwamwitu aliondoka kichwa chini
huku akinong’ona: “Nilikuwa namtania tu...”
Nelson Mandela alifungwa gerezani miaka 27
mfululizo. Alikuwa na jeshi la wafuasi lililokuwa tayari kutoa maisha
kwa ajili yake. Jeshi la Wazulu, Wakhosa na Wanandi lilipopanda mzuka
lililizidi lile la Kimasai. Lakini Mandela alipata kusema: “Elimu ni
silaha yenye nguvu unayoweza kuitumia kuibadilisha dunia.”
Yaani hata kama wangetumia nguvu wakati ule naye
akaachwa huru, bado kungekuwa na uwezekano wa kuzidiwa akili na makaburu
walionuia kumla mwanakondoo.
Patrice Lumumba katika barua yake ya mwisho kwa
mkewe, Pauline aliandika: “Siku moja Historia itajieleza; haitakuwa
Historia inayotolewa Umoja wa Mataifa, Washington, Paris wala Brussels,
bali ni Historia ya Afrika. Siku moja Afrika itaandika Historia yake
yenyewe, Kusini na Kaskazini mwa Jangwa la Sahara kutatukuka.”
Baadhi ya watu walipata shida na filosofia za
wazee wetu. Tutawezaje kufanya haya wanayosema na tumezoea utwana? Kwame
Nkurumah alijibu: “Njia nzuri ya kujifunza uhuru ni kuwa huru.”
Alimaanisha ukitaka kujifunza kuishi, kwanza ishi.
Haile Selassie I Mfalme wa Ethiopia alisema:
“Elimu inaendeleza uwezo wako wa kufikiri; na uwezo huo hukutofautisha
wewe na viumbe wengine. Ni Elimu inayomwezesha mtu kuyatawala mazingira
yake, kuyafanyia kazi na kutumia rasilimali iliyopo kwa usitawi wa
maisha yake. Ufunguo wa maisha bora ni Elimu kwa kuwa mtu huyu hataishi
kwa mkate pekee.”
Martin Luther King, mwanaharakati wa Kiafrika
aliyeuawa Marekani aliiona Elimu kuwa nyenzo inayomwelekeza mtu kufikiri
na kuishi kwa umakini: akili jumlisha tabia yake. Hilo ndilo
alilolisema kuwa ni lengo la elimu ya kweli. Mwanaharakati mwingine
Malcom X alisema Elimu ndiyo hati ya kusafiria kwenda kwenye wakati
ujao, kwa kuwa kesho ipo kwa ajili ya wanaoiandaa kuanzia leo.
Tukubali ama kukataa, lakini ukweli utabaki kuwa
kweli. Hapa haizungumziwi elimu ya propaganda, bali ni ile mtu
anayozaliwa nayo na kuikuza. Hakuna kabila, dini wala taifa linalokataza
mtu kuwa na elimu. Lakini kinachozuiwa ni aina ya elimu unayoichukua.
Wenzetu hadi leo wana matabaka. Zipo familia zilizotukuka na
zipo familia dhalili. Sisi hatuna mambo hayo, ndiyo maana tulipotawaliwa
na kujikomboa tuliamua kuyafuta yale tuliyoambukizwa. Lakini jini
lililotolewa miilini mwetu haliwezi kuondoka kwa urahisi bila kwenda
kuomba msaada kwa majini wenziwe.
Mwalimu Nyerere aliwafafanulia watu wake kwa hili:
“Inawezekana tatizo la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa
kengele shingoni: tabu ni kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo. Pia
panya watakuwa wajinga sana wakidhani kuwa paka watajifunga au
watafungana kengele shingoni.”
Ujinga ni adui mkubwa maendeleo. Unapofanya ujinga
usidhani kuwa unaowafanyia ndiyo pekee watakaoathirika. Uelewe wazi
kuwa hata wewe mwanzisha ujinga hutaendelea hata dunia iache kuzunguka.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment