HATIMA ya makada sita wa CCM walioadhibiwa mwanzoni mwa mwaka jana wakihusishwa kuanza mapema harakati za kuusaka urais wa Tanzania kabla ya wakati uliopangwa na chama hicho tawala, sasa itajulikana mwezi ujao.
Hayo yalielezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa anazungumzia yaliyojadiliwa kwenye kikao cha siku moja cha Kamati Kuu ya chama hicho tawala chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete kilichofanyika mjini hapa.
Alisema muda wa adhabu waliopewa unatarajiwa kumalizika mwezi ujao ambapo baada ya muda huo kwisha, itafanyika tathmini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao.
“Na kama kuna ambao watakutwa hawakuzingatia masharti ya adhabu zao wataongezewa adhabu,” alisema Nnauye.
Kamati hiyo inatarajiwa kukaa kikao chake chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM –Taifa, Philip Mangula.
Baadhi ya makada wa chama hicho waliopewa karipio kali la kutakiwa kuachana na kampeni za mapema za kuwania kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho ni pamoja na mawaziri wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Akitangaza adhabu hiyo Februari 18 mwaka jana mjini Dodoma, Nnauye alisema makada hao, baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.
Alisema: “Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo; Kwamba, wamethibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7) (i).“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.
“Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.“Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:- “Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.” “Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.
“Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya kuwania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.”
Ratiba ya uchaguzi Aidha, CCM imepitisha ratiba ya shughuli za mchakato wa kuwapata viongozi ndani ya dola pamoja na shughuli za kawaida za chama na kalenda yake.
Alisema ratiba kamili ya shughuli za chama kwa wagombea wake bado na kuwataka viongozi na wananchi kuwa watulivu katika kipindi chote wakisubiri mchakato huo kuanza.
“Tulichopitisha ni ratiba ya kawaida ya shughuli za chama na sio ya wagombea wa CCM ambapo mchakato huo utafanyika mwezi wa sita,” alisema.
Kamati Kuu iliyokutana chini ya Rais Kikwete ilijadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sakata la Escow ambapo kimetaka pamoja na serikali kutoa makucha yake, wahusika washughulikiwe pia kichama.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment