Home » » KWA NINI WATANZANIA HAWANA IMANI NA WAGANGA WA JADI?

KWA NINI WATANZANIA HAWANA IMANI NA WAGANGA WA JADI?

 
Katibu wa Chama cha  Waganga wa Tiba AsiliTanzania,Elias Ulaya.  
Kila baada ya hatua chache katika majiji makubwa kama Mwanza, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya na Tanga, si ajabu kukutana na mabango ya biashara ya kutibu nguvu za kiume, kukuza sehemu za uume, kuongeza makalio, akili za darasani, nyota ya maisha na magonjwa ya zinaa.
Matangazo haya yanashamiri huku jamii ikizidi kuwa na hofu la kuongezeka pia kwa mauaji ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi, mauaji yanayoelezwa yanachangiwa na imani za kishirikina tena kwa msaada wa waganga wa jadi.
Ni kwa sababu hii sehemu kubwa ya jamii nchini imeanza kupunguza imani waliyonayo kwa waganga wa jadi ambao zamani walionekana kuwa mbadala wa tiba za kisasa.
Katibu mkuu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili nchini (Chawamauta), Elias Ulaya anataja sababu kuu nne za imani kwa waganga wa jadi kupungua.
Upigaji ramli
Anatoa mfano wa Geita akisema ni moja ya maeneo yenye waganga feki wanaotumia nafasi yao kusababisha mauaji, yakiwamo ya kulipiza kisasi.
Anasema sheria ya tiba asili ya mwaka 2002, inapiga marufuku kwa mganga yeyote kuendesha huduma za kupiga ramli kwa lengo la kutengeneza ushawishi wa tiba zake ili kujipatia fedha.
“Takriban asilimia 90 ya waganga wa jadi tumebaini bado tunaendesha huduma hiyo ya ramli. Hilo ni tatizo kubwa linalosababisha jamii kuendeleza mauaji kwa vikongwe. Lazima jamii ibadilike na kuelimika,” anasema.
Utapeli wa kiini macho
Shughuli za uganga wa jadi zimesambaa mitaani huku wengi wakijitangaza kupitia michezo ya kiini macho.
Ulaya anasema kutokana na ongezeko la waganga nchini, takriban asilimia 60 ya waganga hao wa jadi wamekuwa wakiendesha huduma za kiini macho ili kuvutia wateja.
“Waganga wengi unakuta wamezungukwa na wananchi mitaani wakitoa huduma za kubadili karatasi kuwa fedha au vitu vya thamani halafu wanawatoza fedha.Hali hiyo imeendelea kuondoa imani kwa wananchi kila wanaposikia huduma za waganga wa jadi,’’ anaeleza.
Ulaghai wa mapenzi
Agosti mwaka 2012, Kijiji cha Namabengo Wilaya ya Namtumbo, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Joseph Mapunda alibainika kuishi na mama yake kindoa kwa miaka 10 mfululizo kutokana na ushawishi wa imani za kishirikina alioupata kutoka kwa mganga wa jadi.
Ulaya anasema mbali na tukio hilo, pia kumekuwa na tabia ya waganga kufanya mapenzi na wateja wao kwa kuwalaghai kuwa hiyo ni sehemu ya tiba.
Anasema sheria inapiga marufuku waganga kujihusisha na tabia hizo chafu kwani hakuna ugonjwa unaotibika kwa njia hizo.
“Hali hiyo inajitokeza zaidi kwa waganga waliopo maeneo ya vijijini lakini mjini imekuwa ikijitokeza kwa kiwango fulani. Maeneo ya mijini kinachojitokeza zaidi ni ushawishi wa kuongeza makalio, nyota za mapenzi, kuongeza nguvu za kiume na hata limbwata,” anasema na kuongeza:
“Baadhi ya huduma zinaweza kuongezeka kutokana na ukubwa wa tatizo kwenye jamii lakini kuna wengine wanatumia nafasi hiyo kulaghai Watanzania.”
Ufumbuzi
Ulaya anasema kutokana na mazingira hayo, Chawamauta imeanzisha harakati za kuendesha elimu nchi nzima kupitia wanachama wake 1,420 waliopo mikoa mbalimbali nchini.
“Waganga wote wa jadi wanatakiwa kutambua kuwa huduma yao ni kama huduma nyingine za matibabu ya afya kwenye jamii. Tunahitaji kuirejesha heshima ya huduma kwa waganga wa jadi,” anasema.
“Kwa hivyo, kama ni huduma itolewe na mganga mwenye ujuzi huo na siyo vinginevyo. Elimu ya utekelezaji wa sheria za Serikali ndiyo msingi wa kazi zetu. Kwa mfano, waganga wamepigwa marufuku kuweka mabango lakini bado wanaweka,’’ anasema.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa