Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SIKU chache tangu wananchi waliovamia eneo la Nyantorotoro kutakiwa kuondoka mara moja kumpisha mwekezaji mwenye leseni Majaliwa Maziku kufanya shughuli zake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Joseph Msukuma amewahamasisha kurejea.
Ofisa Madini Mkoa wa Geita, Mhandisi Pius Lobe hivi karibuni aliwaamuru wavamizi hao kumpisha mwekezaji huyo ili aweze kuendesha shughuli zake za uchimbaji wa kokoto kwa kuwa ndiye mwenye vibali.
Mwenyekiti huyo, juzi majira ya majira ya saa tano asubuhi, alikwenda katika eneo hilo akiwa na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho na kuanza kufanya fujo huku wakilazimishwa kuingia ndani ya eneo hilo, wakidai hawajalipwa sitahiki zao.
Wafanyakazi wa mwekezaji waliokutwa wakiendelea na kazi katika eneo hilo, waliamua kutimua mbio mara baada ya wananchi hao kushinikizwa na Mwenyekiti huyo kuingia kwenye eneo hilo na kuendelea kuponda kokoto mpaka watakapolipwa sitahiki zao.
“Jamani mimi kama Mwenyekiti wa CCM nasema msiondoke katika eneo hili, endeleeni kuponda kokoto mpaka mlipwe haki zenu zote na hakuna wa kuwafukuza hata awe nani,” alisema Msukuma.
Baada ya muda mfupi, jeshi la Polisi likiongozwa na Kamanda wa Wilaya (OCD), Geita, Sylvester Ibrahim, walifika na kuamuru wavamizi hao kuondoka mara moja kwa hiyari yao, ambako walikubali kuondoka pamoja na Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake, Injinia Lobe, alisema wao wanafuata sheria inasema nini na si wanasiasa na kwamba huyo Mwenyekiti anawadanganya na atawaingiza matatani kwani watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omary Mangochie, aliwataka wananchi wa eneo hilo kuacha kusikiliza siasa za kiongozi huyo, bali wafuate sheria za nchi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment