Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAJASIRIAMALI wilayani Chato Mkoa wa Geita wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo yenye masharti nafuu zinazotolewa na Benki mbalimbali ili kukuza mitaji yao na maisha yao kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Benki ya CRDB mkoani hapa, Leonard Matley, jana wakati wa kufunga mafunzo ya wiki moja kwa wajasirimali zaidi ya 60. Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kuwafundisha jinsi ya kukopa, kurudisha na kutunza fedha zao kwenye benki hiyo.
Matley, alisema wameamua kufungua tawi la CRDB katika mji mdogo wa Katoro na kutoa mafunzo hayo kutokana na wananchi hao kutokuwa na uelewa mzuri wa kutunza fedha zao kwenye benki, badala yake wanakaa nazo majumbani ambako wamekuwa wakiibiwa kiurahisi.
Aliongeza kuwa watahakikisha wanatoa mikopo kwa wakazi wa mji huo, na kuwaomba kuchangamkia fursa hiyo, kwani mikopo yao ina riba kidogo na ni kwa ajili ya kumsaidia kila Mtanzania.
“Tumesogeza huduma hii karibu ili watu wapate fursa ya kupata mikopo kwa urahisi na yenye masharti nafuu, wajasiriamali wa mji huu chagamkeni mnufaike ili maisha yenu yawe mazuri,” alisema Matley.
Wajasiriamali hao waliohitimu na kutunukiwa vyeti, waliishukuru Benki hiyo na kuongeza kuwa, walikuwa hawajawahi kupata elimu kama hiyo kutoka sehemu yoyote.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment