Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Gari ya Kampuni ya Uchimbaji wa Dhahabu mkoani Geita (GGM) imekamatwa na wakala wa kukamata mali wa Mahakama Kuu jijini Mwanza huku moja ikikimbia baada ya kampuni hiyo kushindwa kulipa deni la zaidi ya shilingi milioni 57.
Gari hiyo aina ya Toyota Hiace yenye namba T258 ilikamatwa jana saa 7 mchana wakati gari hiyo ikielekea kituo cha kazi, taarifa zilidai kuwa GGM ilishindwa kumlipa Peter Daudi kiasi hicho cha fedha ikiwa ni agizo lililotolewa na Mahakama hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima Daudi alisema kuwa alifungua kesi namba 23 ya mwaka huu katika mahakama hiyo na kushinda ambapo mahakama hiyo iliiamuru kampuni hiyo kumlipa stahiki zake kutokana na kumsimamisha kazi kinyemela kwa tuhuma za wizi wa Mafuta.
“Mimi nilikuwa mwajiliwa wa GGM, nimefanya nao kazi kwa muda wa miaka mitano ,ilipofika Agosti, mwaka 2012 nilisimamishwa kazi,” alisema.
Daudi alisema kuwa baada ya kusimamishwa kazi aliamua kwenda mahakamani akisaidiwa na Chama cha Wafanyakazi wa Mgodini (Tamico) ambapo alishinda kesi na kutakiwa kurudishwa kazini na kulipwa stahiki zake zote za mshahara katika kipindi cha siku 42 wakati akiwa nje ya kazi.
“GGM ilishindwa kunilipa ikabidi nirudi mahakamani kukazia hukumu, nikapewa ‘Court Broker’ wakala wa kukamata mali ambao wamekamata magari gari moja na nyingine dereva amekimbia nayo,” alifafanua.
Alisema kuwa baada kukamatwa kwa gari hilo, kampuni hiyo iliamua kulipa shilingi milioni 15 ambacho ni kiasi kidogo na imelipa bila kufuata utaratibu wa kimahakama kwani iliingiza fedha hizo kwenye akaunti yangu,” alisema
Hata hivyo meneja wa mawasiliano wa kampuni hiyo, Tenga Tenga alipohojiwa juu ya tuhuma hizo alisema, kuwa hana taarifa hizo kwa kuwa yuko nje ya kituo cha kazi na kuomba apewe muda ili aweze kufuatilia suala hilo.
“Niko nje ya kituo changu cha kazi naomba nifuatilie halafu nitatoa majibu baadae baada ya kupata taarifa sahihi,” alisema.
Naye Katibu wa Tamico, Paternus Rwechungura ambaye alisimamia kesi hiyo alithibitisha kuwepo kwa kesi hiyo na kwamba mfanyakazi huyo alishinda kesi lakini GGM ikashindwa kulipa kwa muda wa siku 42 walizopewa na mahakama .
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment