CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Magharibi,kimemvua uongozi Katibu wa
chama hicho Jimbo la Geita,Rogers Ruhega, huku kikitengua uamuzi wa
kuwavua uanachama vigogo wake 10 waliotuhumiwa kwa usaliti.
Akizungumza na gazeti
hili kwa njia ya simu jana,Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Magharibi,
Peter Mekele,alithibitisha kuvuliwa madaraka kwa kigogo huyo.
Alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuwepo mashauriano na uongozi wa chama ngazi ya taifa.
"Ni kweli tumemvua
uongozi Katibu wetu wa Jimbo la Geita kutokana na matumizi mabaya ya
madaraka,ambapo ameonekana kutumia cheo chake kuwakandamiza wagombea
wenzake kwa kuwaita wasaliti... lakini pia kikao kilichofanya uamuzi wa
kuwavua wanachama 10 akiwemo diwani viti maalum kata ya Kagu, Malcelina
Simbasasa, hakikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo," alisema.
Alisema, tayari Rogers
amekwishapokea barua hiyo ya kumvua uongozi. Alisema mbali ya uamuzi
huo,pia chama hicho kimesema viongozi wote wa jimbo hilo hawaruhusiwi
kujishughulisha na shughuli zozote za kiuongozi zinazohusiana na
uchaguzi.
Chama hicho sasa kimemteua, Amos Nyanda, kuwa mratibu wa uchaguzi wa jimbo hilo.
Alisema wanachama wote
waliokuwa wamevuliwa uanachama na Kamati tendaji ya jimbo iliyokutana
juzi hivi sasa ni wanachama halali na wana sifa zote za kugombea
nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho.
Kutokana na uamuzi huo
alisema uchaguzi katika jimbo la Geita,ambao umekuwa ukiahirishwa mara
kwa mara sasa utafanyika Agosti 17, mwaka huu.
Juhudi za kumpata Rogers ili kuzungumzia hatua hiyo hazikuzaa matunda,baada ya simu yake ya mkononi kuwa haipatikani.
Hivi karibuni chama
hicho kimekuwa katika hali ya migogoro ambapo baadhi ya wanachama na
viongozi wake wamefikia hatua ya kutuhumiana kusaliti chama huku baadhi
yao wakitajwa kuwa wafuasi wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zitto
Kabwe.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment