Home » » MGOMBEA CHADEMA AWATOLEA WENZIE BASTOLA

MGOMBEA CHADEMA AWATOLEA WENZIE BASTOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Freeman Mbowe
 
Mmoja wa wagombea kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anadaiwa kuwatishia wanachama wenzake kwa bastola baada ya kuibuka makundi yanayohasimiana ndani ya chama hicho.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi katika kitongoji cha Mkoani kwenye viwanja vya ofisi ya serikali ya mtaa, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa uongozi kata ya Kalangalala mjini.

Akithibitisha taarifa hiyo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Kakamba, alimtaja anayedaiwa kuwatishia wenzake kuwa ni Daud Ntinonu.

Walalamikaji katika tukio hilo ni Neema Chozaire (25), Elikana Gideon (30) na Duba Jackson (35).

Walalamikaji hao wamefungua jalada namba GE/RB/5301/2014 la kutishiwa na bastola. ''Ni kweli taarifa ipo na tayari uchunguzi umeanza wa kumtafuta mtuhumiwa…tukimpata tutamhoji na upelelezi ukikamilika tutawasilisha jalada kwa mwanasheria mkuu wa serikali, hilo ndilo jukumu letu,” alisema Kakamba.

Hata hivyo, alisema bastola inayodaiwa kutumika itafahamika baada ya upelelezi kukamilika.

Awali akizungumzia madai hayo, Chozaire alisema tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa 5:30 asubuhi katika mtaa wa Mkoani, baada ya kutokea kutoelewana kati yake na mtuhumiwa pamoja na wapambe wake kwa kutomuunga mkono.

“Wakati watu walipojitokeza kuamua ugomvi, Ntinonu alitoa bastola yake na kunielekeza kichwani, lakini baadhi ya watu waliingilia kati kumzuia,” alisema Chozaire.

Chozaire ambaye ni Mratibu wa Baraza la Vijana mkoa wa Geita (Bavicha), alikiri kuwapo makundi yanayolumbana ndani ya Chadema akihofiwa ni mamluki baada ya kuhamia  chama hicho akitokea CCM.

Akizungumzia tuhuma hizo, Ntononu, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita kabla ya kuhamia Chadema, alikanusha tuhuma hizo.

Malumbano ndani ya chama hicho mkoani hapa, yamechukua sura mpya baada ya uongozi wa kanda kutoa tamko la kumvua uongozi aliyekuwa katibu wake wa wilaya, Rogers Luhega, aliyewania ubunge jimbo la Geita 2010.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa