Home » » BENDERA ALIPIGA NGOMA ISIYO NA MCHEZAJI

BENDERA ALIPIGA NGOMA ISIYO NA MCHEZAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Ninakumbuka mwaka 2010, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Nkaya Bendera alifanya ziara jimboni kwake wakati huo huku akihimiza wadau wa riadha mkoani Tanga kutumia kikamilifu fursa ya Serikali katika kufufua riadha Tanzania.
Kilichonivuta ni ile taarifa yake ya ‘Operesheni Fufua Riadha Tanzania’ ambayo kimsingi inasaidia kuwatayarisha vijana kushiriki mchezo huo.
Ninakumbuka Bendera alikuwa akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Ushauri ya Maendeleo Mkoa wa Tanga.
Alisema: “Serikali kupitia wizara yangu imeanzisha Operesheni Fufua Riadha ili kuuwezesha mchezo huo kuwa hai kama ilivyokuwa siku za nyuma.”
Alisema nia ya serikali ni kuiwezesha Tanzania kuwa katika ramani ya dunia katika mchezo huo kwa kuwa ina wakimbiaji wazuri, lakini wamekosa msukumo wa kutosha.
Alisema kama watapatikana wanariadha wakali, wakaandaliwa na kunolewa vilivyo, wakimbiaji wa Tanzania watakuwa tishio katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Bendera ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alisema, serikali imempa jukumu la kuzunguka nchi nzima kuitangaza operesheni hiyo.
Nakumbuka Rais Jakaya Kikwete aliitaka RT kutayarisha mpango wa maendeleo ili kupatiwa msaada na serikali ikiwamo kocha kutoka nje.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya maendeleo ya riadha yenye kurasa 15, RT ilikuwa inahitaji makocha kutoka nje.
Mbali na hayo, RT ilisema makocha hao watakuwa wakifundisha mbio fupi na vihunzi, mbio za kati na ndefu.
Taarifa hiyo ya mpango wa maendeleo ilisema mpango mzima ni kutengeneza timu ya miruko na mitupo, kuanzishwa kwa kituo cha mazoezi mjini Singida, kuanzisha mashindano maalumu katika mikoa ya Arusha, Singida, Manyara na Dodoma kwa ajili ya kuibua vipaji vya vijana wenye umri chini ya miaka 16 kutoka katika mashindano mbalimbali ya shule.
Lakini pamoja na yote hayo, makocha wa Cuba walipatikana, lakini hakuna kilichosikika kuwa kimefanyika. Hatukusikia programu za vijana kwa shule kama wanavyofanya Ethiopia na Kenya
Hivi hatujiulizi Kenya wanafanyaje, hatujiulizi Ethiopia wanafanyaje hadi kushinda? Siku zote viongozi wa RT wanasubiri safari za Madola, ubingwa wa dunia na Olimpiki na kuja na kapu la visingizio kama ilivyo sasa.
Mashindano wanayojua kuyafanya ni klabu bingwa ya taifa ya riadha na ikiisha hapo wamemaliza. Hawa vijana je?
Kuna mahala Bendera alisema vijana wapo, lakini wanakosa msukumo, sasa ni wazi hili la kuwategemea viongozi wa RT, riadha haitafika popote.
Msukumo wa kweli unahitajika. RT, kamwe hawawezi kutengeneza timu imara za riadha, hawana programu endelevu, sasa hata zikianzishwa operesheni za aina gani hakuna kitu. Si tunaona, kazi yao ni kulalamika tu.
Wenyewe wameshindwa kuziendeleza operesheni walizozianzisha au kuanzishwa. Kulikuwa na operesheni Ikangaa, kulikuwa na operesheni Nyambui, lakini zimekufa.
Usoni kwa RT kulikuwa na Dar Marathoni, iko wapi? Nakumbuka Miradi ya Norway ya Michezo kwa Wote, ilipoanzishwa, kulikuwa na mafanikio, tangu enzi ya TAAA, lakini sasa AT ni kaburi lake.
Ndiyo maana hata Operesheni ya serikali ya Fufua Riadha Tanzania ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa kwani kama ni ngoma inapigwa, lakini hakuna wachezaji.
Hali hiyo ya kukosa wachezaji walioandaliwa vema ilionekana katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyomalizika mjini Glasgow, Scotland na wanamichezo wa Tanzania kutoka kapa, kumaliza mashindano bila medali!
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa