Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUKOSEKANA kwa vyoo vya kutosha katika shule mbili za msingi za
Nyankumbu na Mkombozi zilizoko wilaya ya Geita, mkoani hapa,
kumewalazimu walimu 97 kutumia choo chenye tundu moja, kilichojengwa
katika nyumba anayoishi mmoja wa walimu hao.
Mbali na adha hiyo, pia wanafunzi 3,563 wa shule hizo wanalazimika
kutumia matundu 14 ya choo, hivyo kuzua kero kubwa kwa shule hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Nyankumbu, Jasmin Ngume, alisema shule hizo ambazo awali ilikuwa
moja kabla ya kuigawa zimejikuta zikilazimika kugawana matundu saba
kila shule kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Alisema kawaida na kwa mujibu wa mwongozo wa serikali, uwiano wa
vyoo ni walimu wanne wa kiume kutumia tundu moja na wa kike matatu.
Mwalimu huyo alisema kero hiyo imezua sintofahamu baina ya walimu na
wanafunzi juu ya namna ya kujisaidia kiasi cha kuwalazimisha baadhi ya
watumishi hao kwenda kwenye nyumba za majirani kuomba hifadhi.
Baadhi ya wanafunzi waliliambia Tanzania Daima kuwa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa, kiasi cha kusababisha kukosa umakini katika masomo.
“Kutokana na kukosa vyoo, wakati mwingine tunaogopa kula tukashiba
maana tukihitaji huduma ya vyoo hatutaipata kwa wakati, na hili
linatusababishia tushindwe kusoma vema kwa sababu tuna njaa” alisema
mwanafunzi mmoja aliyekataa kutaja jina lake.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment