Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Polisi mkoani hapa limeanzisha msako mkali wa kuwatafuta
watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi waliovamia familia moja na
kumuua kijana Ng’hayiwa Lengwa (14).
Mbali na mauaji hayo, majambazi hao waliwajeruhi vibaya watu wengine
wanne, kati yao wawili wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na
waliobaki wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Majambazi hao walivamia familia hiyo mwanzoni mwa wiki hii katika
Kijiji cha Kamhanga, wakiwa katika harakati za kusafirisha ng’ombe
waliowaiba katika Kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Wilaya ya
Geita, mmoja wa majeruhi, Kamuli Makono (35), ambaye ni mama wa familia
iliyovamiwa, alisema kuwa yeye na familia yake walivamiwa na watu hao
baada ya kutimuliwa na wananchi usiku wa manane.
“Tulikuwa kwenye sherehe kitongoji jirani kwa mtoto wetu, Shida
Lengwa, na baada ya sherehe kuisha mume wangu na wenzake walirudi
nyumbani, lakini walipokuwa njiani walikutana na watu wawili waliokuwa
wakiswaga kundi la ng’ombe majira ya saa 7 usiku.
“Mume wangu na wenzake walianza kuwahoji wanakotoka na ng’ombe hao,
lakini watu wale walikuja juu ndipo mume wangu na wenzake wakapiga
yowe, ili wawakamate,” alisema mama huyo.
Alidai kuwa baada ya kuona hivyo, majambazi hao walikimbia na
kuziacha ng’ombe hadi kwenye sherehe aliyokuwepo na wakaanza kuwapiga
na kuwakatakata mapanga waliokutana nao hadi kumuua binti yake na
kuwajeruhi Pili Julius, Kamuli Makona, na wageni wawili ambao wamelazwa
Bugando.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya, Adamu Sijaona, alithibitisha
kuwepo kwa wagonjwa hao walioletwa hospitalini hapo huku akieleza kuwa
hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Joseph Konyo, alisema wanaendesha
uchunguzi huo ili kupambana na vitendo vya kijambazi vinavyoelekea
kushamiri mkoani hapa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment