Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Umejikata kwa bati mguuni, lakini unaonekana kutojali ukijua kuwa ni jeraha dogo tu ambalo huhitaji matibabu rasmi ili upone.
Ndivyo ilivyo kwa watu wengi ambao wakipata
majeraha madogo, hupuuza kutumia dawa hufunga kidonda plasta, kutia
dawa za vidonda ama wakienda zahanati hupatiwa tetracycline au amoxicillin kwa ajili ya kuua vijidudu vinavyoweza kupenya kwenye damu.
Kulingana na uzoefu, vidonda vimekuwa vikitibiwa
kwa mazoea lakini ripoti moja ya utafiti wa karibuni inatoa tahadhari
dhidi ya matumizi ya dawa za kiholela.
Shirika la Afya la Dunia (WHO) limetoa ripoti
hivi karibuni na kubaini kuwa dawa zinazotibu maradhi kama kuharisha,
vichomi, maambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI), mafua na magonjwa ya
zinaa kama vile kisonono, kaswende na pangusa zimekuwa sugu.
Ripoti hiyo iliyotolewa Aprili 25 imeeleza kuwa bakteria waenezao maradhi hayo, hivi sasa wanaua kuliko ugonjwa wa Ukimwi ambao hadi sasa hauna tiba madhubuti wala chanjo.
“Ni janga kubwa kuliko Ukimwi ambao umesababisha vifo zaidi ya milioni 25 duniani kote,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Mshauri wa masuala ya usugu wa dawa wa WHO, Dk Lo Fo Wong anaonya na kusema: “kila mmoja yupo hatarini”
Baada ya nchi 114, ikiwamo Tanzania kuthibitika
kuwa na tatizo hilo duniani, Wong alionya kuwa ni lazima fedha ziwekezwe
zaidi katika kutengeneza dawa mpya zinazoweza kutibu magonjwa
yanayosababishwa na bakteria.
Aliyekuwa mkemia mkuu wa Serikali, Dk Juma Madati anasema usugu wa dawa unatengenezwa na mtumiaji mwenyewe.
Anasema ikiwa mgonjwa anapewa dawa na kushindwa
kumaliza dozi au kunywa leo, kesho anaacha na kuendelea tena baada ya
siku kadhaa, basi dawa hutengeneza usugu.
“Ikiwa unapewa halafu humalizi dozi, wale wadudu hushindwa kufa na hugeuza dawa kuwa chakula chao,” anasema.
Anasema usugu wa dawa si katika maradhi yasababishwayo na bakteria pekee hata malaria ipo hivyo. Hata ukipiga sindano ya quinine, kama malaria ikiwa sugu haiwezi kuponya.
“Ndiyo maana hutakiwi kujitibu mwenyewe. Unapoumwa ni lazima
ukatibiwe hospitali na upimwe badala ya kunywa dawa bila kujua unaumwa
nini,” anaonya Dk Madati.
Dk Keiji Fukuda, Mkurugenzi wa Usalama wa Afya wa
WHO alisema bila kuchukua hatua madhubuti, dunia inaelekea katika wakati
ambao yale maradhi ya kawaida ambayo awali yalitibiwa na dawa za
kawaida, sasa yanaweza kuua. Wasiwasi pia umezidi baada ya dawa za
kumaliza virusi kwa mfano wa mafua nazo kukosa uwezo wa kufanya kazi
inavyotakiwa.
Madaktari wengi waliohojiwa katika nchi 114 walikiri kuwa dawa za vijaviuasumu (antibiotic)
hazifanyi kazi kabisa kwa maradhi yanayoathiri ngozi kama vile upele,
fangasi, muwasho, kuathirika kwa mirija ya kupitisha mkojo, kifua kikuu
na kisonono.
“Wasiwasi mkubwa uliopo ni kuwa kuna aina za
ugonjwa wa mapafu ambao ambao umekuwa na usugu wa dawa, ina maana kwamba
watu watakaougua maradhi hayo watapoteza maisha” ilisema ripoti hiyo.
WHO iliuasa ulimwengu kuchukua hatua madhubuti na za awali kama kuosha mikono kuzuia bakteria wasizagae na kuathiri.
Mchunguzi wa Magonjwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, Innocent Mosha anasema maradhi yasababishwayo na bakteria
yapo na yanaua sana.
Anasema bakteria wenyewe huweza kutengeneza vimeng’enyo ambavyo husababisha usugu.
Mfamasia Anna David wa jijini Dar es Salaam
anasema dawa kutengeneza usugu ni kitendo cha kushindwa kutibu au
kuwadhuru bakteria, virusi wanaosababisha maradhi.
Kwa mfano nchini Kenya, ripoti zinaonyesha kuwa
bakteria aina ya ecoli, ambaye husababisha maradhi ya kuhara, kufeli kwa
figo na kukauka kwa damu kwa sasa hatibiki kwa dawa kwa sababu zile
zinazotumika kwa maradhi hayo, Cephalosporins zimeshindwa kutibu.
Hivi sasa madaktari wanalazimika kuwaandikia
wagonjwa dawa za gharama kubwa kama carbapenems ambazo hazipatikini
katika famasi nyingi.
Dawa ya kwanza ya kutibu maambukizi aina ya
penicillin ilitengenezwa na Alexander Fleming, mwaka 1929 lakini uwezo
wake wa kufanya kazi ulianza kushuka miaka ya 1960 na mwaka 1998 na
tayari waraka umetumwa kwa madaktari kuacha kuwaandikia dawa hizo
wagonjwa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment