Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU wanne waliokamatwa kwa tuhuma ya kumkaba na kisha kumnyonga
mwanafunzi wa darasa la pili (jina linahifadhiwa) katika Shule ya
Msingi Kalangalala wameachiwa huru kabla ya kufikishwa mahakamani
katika mazingira ya kutatanisha.
Kuachiwa kwa watuhumiwa hao waliotajwa kwa majina ya Shija Juma,
Dotto Juma na Kulwa Juma, ambao ni ndugu na mwanamke mmoja
aliyejulikana kwa jina moja la Shida, kumewashangaza wananchi wakiwemo
wazazi wa marehemu, huku watendaji wa vyombo vya dola wakikana kuhusika
na jambo hilo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Peki Makoye, akizungumza na Tanzania Daima
Jumatano kwa njia ya simu kutoka jijini Mwanza, alisema kuwa
ameshangazwa kusikia kuwa watuhumiwa hao wako huru wakati wao wakiwa
bado katika msiba.
“Nimeshangaa kusikia kuwa watuhumiwa wako huru, wakati tulikubaliana
polisi kuwa tumalize kwanza msiba ndipo tuweze kuendelea na kesi,”
alisema kwa masikitiko.
Baba wa marehemu, Kilalio Kilalio, alisema kuachiwa kwa watuhumiwa
hao kumezidi kuwaumiza zaidi, na akaomba mamlaka za juu za dola
kuingilia kati ili haki iweze kutendeka.
Hata hivyo, viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa kila mmoja kwa
nyakati tofauti wameonyesha kushangazwa kwao na kukana kuhusika kwa
namna moja ama nyingine na kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Geita mjini (OCS), Chimakula Enock,
alipoulizwa kuhusu kuachiwa kwa watuhumiwa hao, alisema yeye sio
msemaji wa jambo hilo na kwamba watafutwe wasemaji.
Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Sadock Bwire, alipohojiwa na
Tanzania Daima Jumatano juu ya kuachiwa huru kwa watu hao, alionekana
kushangazwa na jambo hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Joseph Konyo, alipoulizwa jambo hilo
kwa njia ya simu, alidai yuko safarini Mwanza na akaelekeza kumwona
kaimu wake, Prudencia Protas, ambaye naye alisema hana taarifa na
akaahidi kulifuatilia ili ajue ukweli wake.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua mtoto huyo Mei 3, mwaka huu katika tukio linalodaiwa kuhusishwa na uhasama wa mapenzi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment