Home » » Serikali yatishia kufuta leseni za wachimba madini

Serikali yatishia kufuta leseni za wachimba madini

 Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini inakusudia kufuta leseni 10 za uchimbaji wa madini katika Mkoa wa Geita kutokana na wamiliki wake kushindwa kutekeleza taratibu na sheria za leseni za uchimbaji kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
Leseni hizo zinazokusudiwa kufutwa ni zile zilizotolewa na Serikali kupitia wizara hiyo mwaka 2008.
Kusudia hilo linakuja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo kutoa notisi ya siku 45 kwa wamiliki wa leseni hizo kujieleza kwa nini wasifutiwe kutokana na kushindwa kufuata sheria hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Geita (GEREMA)kilichofanyika jana kwenye Hoteli ya Katoma, Mtaalamu wa Miamba ya Madini, Moses Sagiko kwa niaba ya Ofisa Madini Mkazi Kanda ya Geita, Juma Sementa, alisema notisi hizo zimetolewa tangu Januari 14, mwaka huu.
Alisema hatua hiyo ya Waziri Muhongo kutoa hati ya kuzifuta leseni hizo ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya madini namba 13(1) ya mwaka 2010, ambapo leseni ya wachimbaji wadogo wanaoshindwa kutekeleza taratibu na sheria za leseni hufutwa.
Sagiko alifafanua kuwa sababu kuu mbili kwa Serikali kukusudia kufuta leseni hizo, moja ni baada ya wamiliki wake kushindwa kuendeleza shughuli za uchimbaji na uzalishaji katika maeneo yao kinyume na kifungu cha sheria Na.52 cha sheria ya madini.
Alisema sababu ya pili ni kushindwa kuchukua hatua mahususi za kulinda na kuendeleza mazingira kinyume cha sheria ya madini kifungu cha 12c na kushindwa kutoa taarifa za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Sagiko alisema mwezi uliopita serikali kupitia ofisi ya waziri Muhongo ilifuta leseni zaidi ya 100 kutokana na wamiliki wake kukiuka taratibu na sheria za leseni za uchimbaji wamadini.
Awali mwenyekiti wa chama cha wachimbaji mkoa wa Geita(GEREMA),Christopher Kadeo alisema wamiliki wa leseni hao wameshindwa kuziendeleza leseni zao kutokana na kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka kwa kuingia mikataba na kampuni za kitapeli.
Kadeo alisema kampuni hizo ziliwarubuni baadhi ya wamiliki wa leseni hizo kubadili leseni zao kutoka leseni za uchimbaji mdogo(PML),kuwa leseni za uchimbaji mkubwa(ML) ili kuingia mikataba bila kujua madhara ambayo yameanza kujitokeza.
Aidha alisema ,GEREMA katika mkutano huo iliwataka wachimbaji hao walioandikiwa hati wajibu hoja za waziri Muhongo na kwamba chama cha wachimbaji mkoa kitakuwa nyuma yao kuhakikisha kinawanusuru wasifutiwe leseni.
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa