JESHI la Polisi wilayani Chato linamshikilia Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Elimu, Paschal Antony kwa mahojiano kwa tuhuma za kuchoma
kaya saba na kuziteketeza kwa moto kwa imani za kishirikina.
Baadhi ya wanakijiji wamekimbia makazi yao baada ya kupata taarifa za
uwepo wa jeshi hilo, huku wengine wakirejea kwa kujifichaficha
wakihofia kukamatwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakeneno, Kata ya Buziku, James Mlomba, amethibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo.
“Inadaiwa Jumapili mwenyekiti huyo alionekana kwenye msiba wa Dagala
Ndilo aliyefiwa na mtoto wake na kisha kuonekana kuwa na kikao na
baadhii ya watu na baada ya muda wananchi waliandamana kwenda kuchoma
nyumba hizo,” alisema Mlomba.
Mtendaji wa kijiji hicho, Emili Mwijarubi, alipoulizwa kuwa
alikamatwa pamoja na mwenyekiti huyo na baadae kuachiwa, alikana na
kusema yeye ndiye aliyetoa taarifa polisi uwepo wa tukio hilo.
Alisema Jumanne iliyopita Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Chato alifika katika eneo lao na kumchukua mwenyekiti huyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaya tano zilichomwa moto na wananchi
kwa madai ya ushirikina na kwamba kabla ya tukio hilo kulikuwa na
mkutano wa kuwapigia kura watu wanaodhaniwa kuwa ni washirikina.
Kaya tano zilichomwa Jumapili, na siku nyingine zilichomwa nyingine mbili.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment