Home » » RAIS KIKWETE ASIKITISHWA NA WATOTO WENGI GEITA KUTOFANYA MTIHANI WA ELIMU YA MSINGI,AAGIZA WATAFUTWE WARUDI SHULE‏

RAIS KIKWETE ASIKITISHWA NA WATOTO WENGI GEITA KUTOFANYA MTIHANI WA ELIMU YA MSINGI,AAGIZA WATAFUTWE WARUDI SHULE‏

-ATOA USHAURI UJENZI WA HOSPITALI YA MKO
 -ATAKA MRADI WA MAJI GEITA UHARAKISHWE
 
Na Marco Kanani, Geita
 
 
 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na idadi kubwa ya wanafunzi mkoani hapa kushindwa kumaliza elimu ya msingi bila kujulikana waliko.
 
Rais Kikwete aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha inawafuatilia wanafunzi wote ambao hawakufanya mtihani mwaka huu watafutwe ili warudishwe shuleni.
 
 
Rais alitoa agizo hilo  jana baada ya kupokea taarifa ya mkoa iliyosomwa kwake na mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula Ikulu ndogo mara baada ya kuwasili mkoani Geita kuanza ziara ya kikazi ya siku tano.
 
Akisoma taarifa hiyo mkuu huyo wa mkoa alisema watoto waliandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2007 ni 52355 na waliofanya mtihani mwaka huu ni 30367 ambao hakumaliza shule wakiwa 21988 hali iliyomshtua sana Rais.
 
Baada ya kusoma takwimu hizi Rais alimkatisha akiwa amehamaki na kusema idadi hiyo ni kubwa hivyo alihitaji aelezwe sababu za watoto hao kutomaliza shule.
 
Mkuu wa mkoa alieleza kuwa sababu zilizochangia watoto hao kutomaliza ni pamoja na mwamko mdogo wa wazazi kielimu pamoja na watoto hao kuajiriwa migodini na wengine kujiajiri kwenye biashara ndogondogo .
 
"Idadi hii ni kubwa mno hili sio suala la kusoma tu bila kutoa majibu ya ufumbuzi wa suala hili ni hatari kubwa kwa ustawi wa Taifa watoto wote hawa kushindwa kuendelea na masomo watafuteni watoto hawa wote na hakikisheni wanarudi shuleni " alisema Rais kwa msisitizo.
 
Akizungumzi asuala la maji katika mji wa Geita  Rais aliutaka uongozi huo wa mkoa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wananchi wa mji huo wanapata maji haraka.
 
Alisema viongozi wote wa idara ya maji wafanye juhudi kubwa na wasikae tu ofisini washughulike ipasavyo badala ya kukaa na kuwa watu wa kutoa taarifa zisizoendana na vitendo.
 
Kuhusu ujenzi wa wa Hospitali ya mkoa wa Geita Rais alishauri ujenzi uende kwa awamu badalaya utaratibu alioelezwa na mkoa wa kusubiri hadi pesa yote ipatikane.
 
"nawashauri kwa kadiri pesa inavyopatikana mwendelee na hatua za ujenzi mnaweza kuanza na OPD, Maabala ,jengo la utawala na baadhi ya wodi kisha mkawa na vyumba vya mionzi lengo nataka muwe na hospitali ya mkoa mapema " alishauri rais.
 
Rais Kikwete aliwasili mkoani hapa jana katika uwanja wA Ndege wa GGM majira ya saa tano na nusu na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa mkoa wakiwemo viongozi wa dini .
 
Akiwa mkoani Geita Rais amezindua rasmi mkoa huo uzinduzi ambao umefanyika katika uwanja wa CCM Kalangalala kisha alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uwanjani hapo kabla ya kuelekea Chato jioni.

Geita yetu Blog

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa