Home » » JK asisitiza wachimbaji wadogo kusaidiwa

JK asisitiza wachimbaji wadogo kusaidiwa


Rais Jakaya Kikwete
 
Serikali imesisitiza kuwa itawasaidia wachimbaji wadogo ikiwamo kuwapatia leseni na maeneo ya uchimbaji kwa watakaofuata taratibu za kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Rais Jakaya Kikwete wakati akifungua mgodi mdogo wa Nsagali Gold Mine (NGM) unaomilikiwa na mwekezaji mzawa,  Emmanuel Gungu katika mji wa Ushirombo.

Alisema serikali haitaacha kumsaidia mchimbaji mdogo hasa katika kumpatia mitambo ya  kufanya shughuli za uchimbaji ili afanye kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Mmoja wa wakurugenzi wa mgodi huo,  Njalu Silanga, alisema ujenzi wake umegharimu Sh. bilioni 3.3 na unasaidia jamii katika sekta ya elimu na maji katika eneo uliopo la Katente.
Alisema mgodi huo ambao unazalisha tani 120 za mawe na kusagwa kwa siku, utakuwa ukinunua mchanga wa marudio kutoka kwa wachimbaji wadogo na kuurudia kwa mara ya pili kitaalamu ili kupata malighafi inayohitajika.

Hata hivyo,  Silanga alisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa umeme hali ambayo inafanya uzalishaji kuwa mdogo kutokana na kutumia jenereta.

Rais Kikwete yuko katika ziara mkoani Geita na mawaziri John Magufuli (Ujenzi),  Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Naibu Waziri  Stephen Masele (Nishati na Madini), Naibu Waziri , Kassim Majaliwa (Tamisemi) na maofisa mbalimbali wa serikali.

Akiwahutubia wakazi wa mji wa Ushirombo alisema kama kuna mfugaji ambaye ng’ombe wake wamepigwa risasi na askari wa wanyamapori katika operesheni Tokomeza, serikali haitasita kuwachulia hatua wahusika.

Alisema kwa sasa kiwango cha uwindaji wa wanyamapori kimefikia kiwango cha kutisha hali ambayo serikali haiwezi kuvumilia uharamia huo na kuongeza kuwa katika hifadhi siyo mahali pa kulishia ng’ombe bali  wanyama pori.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa