Picha ya Bi.Aziza Ramadhani akiwa na jeraha baada ya kuvamiwa na majambazi
,Denice Stephano,Geita
Yetu
Siku tatu baada ya mtoto
Shaban Maulid (15) aliyedaiwa kufariki kisha kuonekana akiwa hai mwishoni mwa
mwezi jana, kuruhusiwa hospitalini alikokuwa amelazwa,watu wasiojulikana
wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia nyumbani kwao mtaa wa 14 Kambarage mjini
hapa na kumjeruhi mama wa mtoto huyo baada ya kumpora fedha aliyokuwa
amechangiwa na wasamaria wema wakati akimtibisha mwanaye.
Mama wa mtoto huyo Aziza
Ramadhan (45) alivamiwa usiku wa manane wa kuamkia leo kisha kuporwa fedha
taslimu tsh 210,000 ambayo ilikuwa michango aliyopewa na wasamaria wema wakati
akimuuguza mtoto wake katika hospitali ya wilaya ya Geita.
Imedaiwa na majirani wa
mama huyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini kuwa majambazi hao
walivamia nyumbani kwa mama huyo majira ya saa tisa usiku ambapo walipiga
mlango kwa jiwe kubwa maarufu kama fatuma kisha kuingia ndani.
Watu wao waliokuwa na
siraha za jadi walimweka mama huyo chini ya ulinzi huku wakimtaka awape pesa
alizokuwa akichangiwa hospitali ndipo alipowapa kiasi laki mbili na elfu kumi
ambacho walidai ni kidogo mno na kumtaka aongeze.
Baada ya kujitetea kwao
kuwa hana pesa nyingine walimjeruhi kichwani kwa kitu chenye ncha kali na
kusababisha jeraha kichwani na kulazimika kukimbazwa hospitali kwa matibabu
zaidi.
Akizungumzia tukio hili
Afisa mtendaji wa kata ya Kalangalala Bw.Hamad Hussen amesema usiku wa kuamkia
leo familia zipatazo kumi zimevamiwa na watu hao na kuporwa fedha pamoja na
vitu mbalimbali
Aliwataja baadhi ya watu
waliovamiwa na kujeruhiwa kuwa Peter Kulwa(24) Maneno Sungura(32) wote wakazi
wa mtaa wa 14 Kambarage ambao walitibiwa hospitali na kuruhusiwa
Akiongea na mwandishi wa
habari hizi Kaimu mganga mfawidhi Dr,George Rweyemera alisema
walifikishwa watu watatu hospitalini hapo alfajiri ambapo walitibiwa
kisha waliruhusiwa kurudi nyumbani kutokana na hali zao kutokuwa mbaya.
"Aziza alifika hapa
majira ya saa kumi na moja alfajiri akiwa na jeraha kichwani,alihuhumiwa na
kupatiwa dawa na tumemruhusu maana hakuwa ameumia sana" alisema Dr.George
Hata hivyo baadhi ya
majirani walioongea na mwandishi wa habari hizi walionesha wasiwasi wao kuwa
huenda watu hao walilenga kumdhuru mtoto huyo ambaye alikuwa ameruhusiwa kutoka
hospitali juzi .
"Inawezekana hawa
watu walikuja kumchukua Shaban ila wakamkosa ndio wakadai pesa kama lengo la
uvamizi huo" alisema mmoja wa majirani.
Hata hivyo mtoto
Shaban hayupo nyumbani kwao akidaiwa kuondoka na baba yake Maulid Shaban
na kuhifadhiwa sehemu ambayo imedaiwa ni siri ya familia wakati
wakisubiri majibu vinasaba (DNA) kutoka kwa mkemia mkuu wa serikali.
Shaban alifariki Januari
Mosi 2011 na kuzikwa kisha kuonekana akiwa hai baada ya kukutana na mama
yake Septemba, 30 mwaka huu tokea wakati huo alikuwa akipata huduma ya kitabibu
na ya kisaikolojia katika hosipitali ya wilaya ya Geita hadi Okitoba 10
aliporuhusiwa kwenda nyumbani.
Jitihada za kumtafuta
kamanda wa polisi mkoa wa Geita Leonard Paulo hazikuzaa matunda na alipopigiwa
simu kupitia simu yake ya kiganjani ili kuthibitisha tukio hilo alisema
hayuko sehemu nzuri.
"siko sehemu nzuri
kwasasa haloo.....eeeh siko sehemu nzurii!" alijibu Kamanda
Aidha jeshi la polisi
wilaya ya Geita wamekiri kutokea kwa tukio hilo na kudai uchunguzi wa tukio
hilo unaendelea.
0 comments:
Post a Comment