Home » » WANANCHI WAFUNGA OFISI YA KIJIJI

WANANCHI WAFUNGA OFISI YA KIJIJI



na Victor Eliud, Geita
OFISI ya Serikali ya Kijiji cha Mpomvu Kata ya Mtakuja wilayani Geita, katika Mkoa mpya wa Geita, imefungwa na wananchi kutokana na viongozi wa kijiji hicho kutuhumiwa, akiwemo ofisa mtendaji Kavula Sitta, kujihusisha na ufisadi.
Wananchi zaidi ya 200 waliandamana juzi majira ya saa 10:00 jioni hadi ilipo ofisi hiyo na kisha kuifunga kwa kile walichodai Sitta kushindwa kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka mzima huku baadhi ya fedha za kijiji hicho zikiishia mfukoni.
Walidai kuwa mtendaji huyo kwa kushirikiana na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho, wamekuwa wakitafuna fedha hizo zinazopatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ya kijijini hapo ikiwemo viingilio vya mashine za kusaga mawe ya dhahabu na viingilio vya wageni.
Walidai kuwa baadhi ya wananchi wanaohamia kijijini hapo hutozwa sh 60,000 kama kiingilio lakini cha kushangaza fedha hizo hazifikishwi benki ili kuingizwa kwenye akaunti ya kijiji na matokeo yake yanaishia mifukoni mwa baadhi ya viongozi hao.
Kufungwa kwa ofisi hiyo kumefanya shughuli za serikali zisimame kwa muda sasa tangu Oktoba 20, mwaka huu, huku wakisisitiza kuwa hawatafungua ofisi hiyo hadi pale serikali itakapopeleka wakaguzi na kufanya uchaguzi mpya wa wajumbe.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Balenge Kwitega, alithibitisha kufungwa kwa ofisi hiyo na kukiri wazi kuwa hana taarifa za mapato na matumizi zilizowahi kusomwa kijijini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Mangochie, alipoulizwa juu ya taarifa hizo hakukiri wala kukanusha na badala yake aliliomba gazeti hili kufika ofisini kwake
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa