na Victor Eliud, Geita
MIKUTANO
ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), imetikisa Jimbo la Busanda, wilayani Geita, mkoani Geita,
baada ya wanachama 18,670 wakiwamo wazee na makada wa siku nyingi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kutimkia CHADEMA.
Mbali
na kuzoa maelfu ya wanachama, pia chama hicho kimeunda uongozi kwa kuteua
wenyeviti, makatibu, na wahazini wa chama kwenye kila kata zilizokuwa hazina
uongozi ngazi ya tawi.
Viongozi
waliosimikwa ni wenyeviti, makatibu, wenezi na wahazini wa matawi pamoja na
wale wa jumuiya mbalimbali za chama hicho hususan wazee (BAWAWACHA), Vijana
(BAVICHA) na Wanawake (BAWACHA), lengo likiwa ni kukiimarisha chama kuelekea
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake kwenye
jimbo hilo juzi, Kiongozi wa M4C mkoani Geita, Alphonce Mawazo, alisema wana
CCM waliojiunga na chama hicho ni kutoka kata 13 kati ya 16 za jimbo hilo.
Alisema
kati yao 11,235 ni wanachama wapya na 7,435 ni waliovua gamba na kuvaa gwanda,
ili kuhakikisha CHADEMA kinaibwaga CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na
kuingia Ikulu.
Aliwataja
miongoni mwa wazee na makada wa siku nyingi wa CCM waliorudisha kadi za CCM ni
Thereza Lugembe (79) mkazi wa Kijiji cha Nyabulolo, Kwando Maduhu (109) mkazi
wa Kijiji cha Nyarugusu na Shija Mihambo (87) mkazi wa Bugogo Bukoli ambaye
alikuwa mwanachama wa CCM tangu Julai 7, mwaka 1979 kwa kadi namba C.812836.
“Kazi
hii si ndogo…tunapambana na chama ambacho kina mizizi kila kona…tumezoea kuona
vijana ndio wanajiunga na CHADEMA…lakini unapoona wazee nao wameanza kukimbia
ujue saa ya ukombozi imekaribia,” alisema Mawazo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment