Home » » Jela maisha kwa kubaka, kuambukiza ukimwi

Jela maisha kwa kubaka, kuambukiza ukimwi



na Ali Lityawi, Geita
MAHAKAMA ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imewahukumu kifungo cha maisha vijana wawili kwa makosa mawili ya ubakaji na kumuambukiza ugonjwa wa ukimwi mtoto wa miaka minne.
Akitoa hukumu hizo kwa nyakati tofauti, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ushindi Swalo, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa huku mmoja wa watuhumiwa hao akikiri kutenda kosa hilo la kumbaka mtoto wa miaka minne.
Katika tukio la kwanza, Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo, Zephania Mnisi, alisema kuwa Desemba 21 mwaka jana, mshitakiwa Revocatus Mihayo (25) alimbaka mtoto wa miaka minne katika Kijiji cha Msonga wilayani Bukombe.
Mnisi aliiambia mahakama hiyo kuwa katika tukio hilo, Mihayo alikamatwa akiwa amempakata mtoto huyo mapajani, huku akimbaka na uchunguzi wa awali wa daktari ulionesha alikuwa ameharibika sehemu zake za siri.
Alisema wakati kesi hiyo ikiendelea na miezi kadhaa ikipita, mtoto huyo alifanyiwa uchunguzi wa daktari kwa mara ya pili na kubainika tayari ameambukizwa virusi vya ukimwi, shitaka ambalo liliongezwa kwenye kesi yake ya msingi ya ubakaji.
Katika shtaka la pili, Shija Marko (18) mkazi wa Lulembera anadaiwa kumbaka mtoto wa miaka minne baada ya kukutana naye shambani wakati mtuhumiwa akiwa na shughuli za kilimo.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa, katika tukio hilo mtoto huyo alipita shambani kwa Marko akiwa uchi wa mnyama jambo ambalo kijijini ni kawaida, lakini mshitakiwa alimshika na kumlaza kwenye matuta na kuanza kumbaka.
Hata hivyo mshitakiwa Marko alikiri papo hapo kutenda kosa lake na kumfanya hakimu Swalo, amhukumu kifungo cha maisha kwa kosa hilo.
Akitoa adhabu hizo kwa nyakati tofauti kwa washtakiwa hao wawili, Mihayo na Marko, hakimu Swalo alisema kwa kuwa washitakiwa wametenda makosa ya kubaka watoto chini ya umri wa miaka kumi, kifungo cha miaka 30 na viboko 12 kimejifuta na sasa watatumikia kifungo cha maisha ili liwe funzo kwa vijana wengine.
CHANZO TANZANIA DAIMA


0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa