Home » » ZIARA YA WAZIRI PINDA MKOANI GEITA

ZIARA YA WAZIRI PINDA MKOANI GEITA

Na David Azaria wa Geita Yetu
WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita ambapo pamoja na mambo mengine atakagua, kufungua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi Mwandamizi wa serikali tangu shughuli za kiserikali kuanza rasmi katika mkoa wa Geita, ambapo Waziri Mkuu anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya wachimbaji wadogo wa dhahabu inayodaiwa kuwa na migogoro.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Said Magalula Said,Lengo la ziara hiyo ya Waziri Mkuu katika mkoa huo ni pamoja na kuangalia namna shughuli za kiserikali zilivyoanza kutekelezwa katika mkoa huo,sanjari na kukutana na wananchi wa kijiji cha Mgusu ambao walifungiwa shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na waziri huyo.
 Machimbo hayo yalifungwa kwa Amri ya Waziri Mkuu Pinda Mei 2,Mwaka 2009 ikiwa ni siku chache baada kutokea vifo vya wachimbaji tisa waliofukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba dhahabu kwenye shimo lenye zaidi ya urefu wa futi 100.
Katika tukio hilo hakuna mwili wa mtu hata mmoja ulioopolewa kutoka ndani ya shimo hilo pamoja na shughuli za uokoaji kudumu kwa siku sita mfululizo,hatua iliyopelekea serikali kuamuru marehemu kuzikwa katika shimo hilo na kisha baadaye kufunga shughuli za uchimbaji.
Kwa mujibu wa Magalula Waziri Pinda ataingia mkoani hapa leo (Jumapili) na kupokelewa  katika wilaya mpya ya Nyang’hwale akitokea Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ambapo atapokea taarifa ya Mkoa kabla ya kufungua vyumba vitatu vya maabara katika shule ya sekondari Nyang’hwale.  
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magalula alisema Waziri mkuu siku ya jumatatu atakuwa wilayani Geita ambapo pamoja na mambo mengine atazindua mradi wa ufugaji nyuki katika kijiji cha Bugulula, na kliniki ya baba,mama na mtoto iliyopo Senga,na kufanya mkutano wa hadhara mjini Katoro.
 Aidha katika ziara hiyo yenye lengo la kukagua na kuhimiza wananchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo akiwa wilayani Geita waziri mkuu atakabidhi Matrekta makubwa tisa kwa watu binafsi na vyama vya ushirika kwa ajili ya shughuli  za kilimo.katika kijiji cha Katoro.
"Hii ni nafasi kubwa sana ya kutembelewa na kiongozi wa kitaifa na pia kutembelewa huko kutasukuma shughuli za kimaendeleo katika mkoa wetu na hasa ukiangalia ataenda katika Wilaya mpya ya Nyang’hwale kwa hiyo wananchi wajitokeze kwa wingi ili tusukume pamoja gurudumu la maendeleo"alisema. Magalula
Ujio wa Waziri Mkuu katika Mkoa wa Geita umekuwa faraja kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Mgusu huku kila mmoja akiwa na hisia tofauti kama atayafungua machimbo hayo au lah, kutokana na kwamba wakazi hao wamekuwa wakiishi maisha ya shida kwa kipindi cha miaka mitatu kufuatia kufungwa shughuli za uchimbaji.
“Tunamsubiri kwa ahamu kubwa na kwa sababu tayari tumehakikishiwa kwamba anakuja kwenye kijiji chetu hiki,tuna imani kubwa kwamba atakuja kufungua machimbo yetu ili tuendelee na shughuli za uchimbaji kwa sababu ndiyo shughuli zetu tunazozitegemea katika kuendesha maisha yetu ya kila siku….’’ Alisema mmoja wa wachimbaji wadogo Robert Otieno.
Aliongeza “unajua kwa sasa tangu kufungwa kwa yale machimbo tumekuwa watu wa kushinda huku mjini bila shughuli yoyote,labda mpaka ubahatishe ukisikia kwamba mahali Fulani kama huko Nyarugusu,Lwamgasa au Nyakagwe kuna dhahabu ndipo ukimbilie kwenda kufanya kazi,lakini kule mgusu tulishazoea ni mahali ambapo kupata dhahabu kila siku ni lazima na hivyo kuwa na uhakikisha wa kuishi…..’’.
Kwa muda Mrefu wachimbaji wadogowadogo wa dhahabu wilayani Geita wamekuwa wakihangaika kupata maeneo ya uchimbaji kutokana na maeneo yao mengi kuchukuliwa na wawekezaji wakubwa kwa ajili ya uchimbaji ama utafiti.
Aidha Mkuu huyo alisema kuwa kwa sasa Mkoa wa Geita umefanikiwa kuthibiti baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiukabili mkoa huo ikiwemo ajali za barabarani,mauaji ya vikongwe uharifu wa kutumia silaha kutokana na kuimalisha hali ya ulinzi na usalama kwa wananchi.
Magalula alisema hata hivyo bado mkoa huo unakabiliwa na tatizo la huduma ya maji safi na salama na  uhaba wa chakula hasa kwa wakazi wa wilaya ya Nyang’hwale kutokana na mazao waliyolima katika msimu wa kilimo uliopita kukaushwa na jua.
Blogzamikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa