Home » » KIONGOZI WA MWENGE AMGWAYA DC

KIONGOZI WA MWENGE AMGWAYA DC

na Victor Eliud, Geita
KATIKA hali inayoonesha nidhamu ya woga, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Kapteni Honest Mwanossa, amemsafisha Mkuu wa Wilaya (DC) ya Geita, Manzie Mangochie mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, kuhusu kudaiwa kupoteza msafara wa mwenge wilayani kwake.
Kapteni Mwanossa alimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa taarifa alizozisikia katika vyombo vya habari ni za uzushi na hakuna mradi uliopitilizwa ingawa alikiri kuwepo kwa mradi huo aliodai kwamba baadaye ulifutwa katika ratiba.
Mwanossa alitoa kauli hiyo wakati akitoa shukrani zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita katika viwanja vya Shule ya Msingi Chato kabla ya kuendelea na mbio hizo katika Mkoa wa Kagera.
“Baba yangu, Mkuu wa Mkoa Magalula, uliyoyasikia sio ya ukweli, tumekimbiza vizuri mwenge wetu wa uhuru katika Wilaya ya Geita, ule mradi ulikuwepo, lakini kumbe ulifutwa kwenye ratiba kwa hiyo hakuna kilichoharibika… tumeshirikiana vizuri, uliyoyasikia ni ya kupuuza,’’ alisema Mwanossa na kusababisha miguno kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwapo kwenye ziara hiyo mkoani Geita.
Mbio za mwenge wilayani Geita ziliingia dosari baada ya Mangochie kuupoteza msafara, hatua iliyosababisha mradi wa kikundi cha kuweka na kukopa uliotarajiwa kukaguliwa kupitilizwa.
Tukio hilo lilitokea Agosti 26 mwaka huu, hali iliyosababisha msafara huo kusimama njiani kwa muda wa dakika 10 katika Kijiji cha Ngula, Kata ya Nyakagwe, kitendo kilichomkera Mwanossa na kutoa karipio kali kwa mkuu huyo wa wilaya.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa