na Mwandishi wetu, Geita
MKUU wa Wilaya (DC) ya Geita, Manzie Omari, ametangaza kupambana kufa na kupona na mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Victor Eliud, kwa madai ya kumchafua.
Pia, amemtishia maisha mwandishi huyo akisema atakiona cha moto ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani kama hatakoma kile alichokiita kuandikwa vibaya katika baadhi ya tuhuma zinazomkabili.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo siku chache baada ya gazeti hili kuchapisha habari iliyokuwa na kichwa kisemacho“CUF wamshitaki DC kwa RC”, ikinukuu barua ya chama hicho kwenda kwa RC Magalula kuelezea namna ya utawala wa mkuu huyo wa wilaya ulivyo wa kibabaishaji, hivyo yeye kusema ililenga kumchafua.
Katika mazungumzo ya njia ya simu Agosti 23 mwaka huu, yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 20, mkuu huyo wa wilaya hakutaka kumpa nafasi ya kuzungumza mwandishi huyo isipokuwa kumshambulia moja kwa moja.
“Hivi wewe Victor unanitafuta nini? Unadiriki kutumia kalamu yako kunichafua siyo? Unatumiwa na huyo kiongozi wa CUF kunichafua mimi. Nataka kukueleza nimekuwa DC kwa muda mrefu wala sikuanzia hapa (Geita). Mwambie huyo Malugu kwamba ofisi yangu haina muda wa kujibu barua zake.
“Na kama huyo Malugu ana ndoto za kuwa DC, mwambie hataupata hadi anaingia kaburini. Hakuna rais wa kumteua akae akijua,” alisema.
Mbali ya hayo, DC huyo alimweleza mwandishi huyo kuwa kuanzia sasa, ni adui yake na kwamba hataki kushirikiana naye kwa namna yoyote ile.
Chanzo: Tanzania Diama
0 comments:
Post a Comment