Home » » RC AWAJIA JUU WATENDAJI CHATO

RC AWAJIA JUU WATENDAJI CHATO

Na David Azaria, Geita Yetu
 
SERIKALI mkoani Geita imewatahadharisha watumishi wa idara ya fedha wa halmashauri ya wilaya ya chato kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali yanayolenga kuwanufaisha watu wachache huku miradi ya maendeleo ikidaiwa kushindwa kukamilika kwa wakati.
 
Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula wakati akizungumza na madiwani wa halmashauri ya chato ambapo alisema idara hiyo imekuwa ikisababisha kuwepo kwa hoja nyingi ambazo hazijafungwa na kusababisha halmashauri hiyo kuendelea kupata hati zenye mashaka kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
 
“Tatizo kubwa lipo hapa kwenye idara ya fedha…maana watumishi wa idara hii wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea…inakuwaje wakaguzi wafike kukagua halafu viambatanisho vikose kama kweli kumefanyika malipo halali?”alihoji Mgalula.
 
Katika taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa Hesabu za serikali CAG inaonyesha kuwa halmashauri ya chato ilikuwa na hoja za nyuma 21 ambazo hazijafungwa,zenye thamani ya shilingi 598.4 na hoja nyingi zilitokana na kutokuwepo kwa viambatanisho vya malipo ya fedha za serikali.
 
“Mheshimiwa mwenyekiti,ninapenda kukuhakikishia kuwa kwa sasa serikali yangu haitakuwa na simile na mtumishi yoyote atakayeisababishia hoja halmashauri hii…lazima tuwakamate na kuwashitaki kwa majina yao wenyewe…hii niaibu kubwa kila mwaka mnapata hati yenye mashaka nasema imetosha”alisema.
 
Magalula alitaja baadhi ya mambo yaliyobainika katika ukaguzi wa CAG kwenye hesabu za halmashauri hiyo kuwa ni kufanya malipo kinyume cha masharti ya mkataba,Manunuzi pasipo kushindanisha zabuni,malipo kabla ya kazi na kukosekana kwa nyaraka mhimu zinazodhihirisha kufanyka malipo halali.
 
Hata hivyo Magalula alitumia nafasi hiyo kunusuru kikao cha madiwani hao ambacho kilitaka kuvunjika kwa mara ya pili mfululizo,baada ya kile cha awali kilichotakiwa kukaa wiki iliyopita kusambaratika kutokana na madiwani hao kutoridhishwa na majibu ya menejimenti yaliyoandaliwa kujibu hoja za ukaguzi wa ripoti ya CAG.
 
Hatua hiyo ilikuja baada ya diwani wa kata ya Ilemela Ismail Luge (CCM) kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo Charles Maisha kukivunja kikao hicho kutokana na kile alichodai majibu ya menejimenti hayakuonyesha hatua zilizochukuliwa kwa watumishi waliohujumu fedha za serikali na mikakati iliyoandaliwa kwa mtumishi atakayeisababishia halmashauri hiyo hoja mpya.
 
“Mheshimiwa mwenyekiti mimi ninaona majibu yaliyotolewa na menejimenti hayaridhishi hata kidogo…iweje tusionyeshwe hatua zilizochukuliwa kwa watumishi waliotusababishia hoja kutokana na maslahi yao binafsi wala mikakati iliyoandaliwa kwa watakaoisababishia halmashauri yetu hoja mpya?”alihoji Luge.
 
Aidha baadhi ya madiwani hao walimnyooshea kidole kaimu mweka hazina wa halmashauri hiyo Fulmence Kishenyi kushindwa kuisimamia vizuri idara ya fedha na kusababisha ongezeko la hoja za kujibu.
 
Diwani wa kata ya Buseresere Chrispine Kagoma (Chadema) aliwataka madiwani hao kuweka kando tofauti zao za kisiasa pindi wanapo ingia kwenye vikao vya kujadili mambo mbalimbali ya halmashauri hiyo yanayolenga kuboresha maendeleo ya wananchi na kupunguza umaskini katika jamii.
 
Kagoma alisema uwepo wa hoja nyingi kwenye halmashauri hiyo ikilinganishwa na halmashauri zingine za mkoa wa geita zinatokana na baadhi ya madiwani wa CCM kupinga hoja za madiwani wa upinzani pindi wanapohoji upotevu wa baadhi ya fedha za miradi ya maendeleo ambapo hupuuzwa na kuzomewa ili kuwadhoofisha.
 Blogzamikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa