Na David Azaria, Geita Yetu.
KIONGOZI wa mbio za mwenge mwaka 2012 Kapteni Honest Mwanossa amesema wabunge wanaotegemea kubebwa na Mwenge wa uhuru kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ‘wameula’ wa chuya kwani kazi hiyo haitafanywa na Mwenye katika kipindi hicho.
Mwanossa alilazimika kutoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo wa uhuru kati ya Mkoa wa Geita na Kagera katika kijiji cha Kasozibakaya wilayani Biharamulo Mkoani Kagera,baada ya kutoridhishwa na ushiriki wa wabunge katika mbio hizo.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa wakati wa mbio hizo katika mwaka wa uchaguzi wabunge wengi huzitumia kujiweka sawa kwa ajili ya uchaguzi na kwamba imekuwa sehemu ya kampeni zao kwa kushiriki mbio hizo kwa silimia 100 huku wakilazimisha kupewa nafasi ya kuzungumza kwenye mbio hizo.
“Cha ajabu ni kwamba kwa sababu wabunge wanajua kwamba huu si mwaka wa uchaguzi ushiriki wao kwenye mbio za mwaka huu umekuwa mdogo sana,na wengi wao hawakushiriki kabisa tena bila hata kutoa sababu….na mwenge wa uhuru nao unasema hakuna tabu wao waendelee kuuytenmga tu lakini kuna siku inakuja………’’ alisema Kapteni Mwanossa na kuongeza.
“Najua wanaubiri mwaka wa uchaguzi ili mwenge uwabebe,nataka kuwathibitishia kwamba hilo halitakuwepo kwa mwaka 2015,watanzania kwa sasa wanataka viongozi wanaowajibika kwa wananchi lakini sio wale wanaoonekana wakati war aha tu na si wakati wa shida,wakija kwenu wakati huo kwa sababu mnawafahamu msiwakubalie na ukifika wakati wa uchaguzi msiwape kura……’’.
Akitoa mfano katika mikoa ya Mwanza na Geita Kapteni Mwanossa alisema wabunge walioshiriki kwenye mbio hizo kwa asilimia 100 ni watatu ambapo katika mkoa wa mwanza wenye jumla ya wabunge 10 ni wawili tu ndio walioshiriki kwenye mbio hizo wakati katika Mkoa wa Geita wenye wabunge 8 ni mmoja pekee ndiye aliyeshiriki kwenye mbio hizo kwa silimia 100.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Mbunge wa jimbo la Misungwi na Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Charles Kitwanga,Mbunge wa Jimbo la Sengerema William Ngeleja kutoka Mkoa wa Mwanza na Augistine Masele Mbunge wa Jimbo la Mbogwe katika Mkoa wa Geita.
“Safari hii kwa sababu wanajua sio mwaka wa uchaguzi wameamua kuutelekeza Mwenge wetu wa uhuru,na taarifa tulizonazo wengine wala hawako kwenye kazi maalum lakini wameamua kwa makusudi kuacha kuja kushirikiana na wananchi wao katika kuukimbiza mwenge wa uhuru,subirini mwaka 2015 ambao utakuwa ni mwaka wa uchaguzi watakavyojazana kwenye mbio za mwenge…..’’ alisema.
Aliongeza “Mwenge wa uhuru wenyewe upo,utaendelea kuwepo na utakuwepo mwaka huo wa 2015,isipokuwa wanaoukimbiza ndio watakuwa wamebadilika,lakini nataka niwaambie kwamba huu mwenge wa uhuru mnaouona hautawabeba hata kidogo,waache waususie sasa hivi ……’’.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa mbio za menge kitaifa mwaka huu aliwaonya watu wote ambao wamekuwa wakibeza mbio za mwenge,na kueleza kwamba mbio hizo ni kichocheo kikuu cha maendeleo kwa vile zimekuwa zikisababisha hata kutengenezwa barabara hata mahali ambapo hakukuwa na bajeti ya kufanya hivyo kwa wakati huo.
blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment