na Sitta Tumma, Geita
SAKATA la
sheria mpya ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii nchini (SSRA), limeanza kuchukuwa
sura mpya, ambapo wafanyakazi wa mgodi wa Geita Gold Mining (GGM),
wameicharukia serikali wakiitaka iwatimue Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka na Mkurugenzi wa Mamlaka ya SSRA.
Mbali na
kuwataka viongozi hao wajiuzulu pia wafanyakazi hao wameitaka serikali pamoja
na Bunge kuhakikisha kipengele cha fao la kujitoa kinaondolewa katika sheria
hiyo namba 5 na si vinginevyo.
Tamko hilo
limetolewa juzi jioni na mwenyekiti wa kamati teule ya kufuatilia na kupinga
uundwaji wa sheria hiyo, Deogratias Haule, katika kikao cha pamoja baina ya
wafanyakazi hao.
Kwa mujibu wa
Haule, kupitishwa kwa sheria na kipengele hicho, kumeonyesha dhahiri kwamba
serikali haina nia njema na wananchi wake, hivyo ni vema Waziri Kabaka na
Mkurugenzi wa SSRA wakaachia ngazi kwani ndiyo waliohusika kuitunga sheria hiyo
kandamizi na dhalimu.
“Kulingana na
utata wa sheria hii inayoonekana kupora fedha na haki zetu, sisi wafanyakazi wa
sekta binafsi hatuna imani tena na Waziri wa Kazi na Ajira pamoja na Mkurugenzi
Mkuu wa SSRA, tunawataka wajiuzulu mara moja nyadhifa zao,” alisema.
Kwa makusudi
Waziri Kabaka na Mkurugenzi wa SSRA, waliamua kufunika kombe mwanaharamu apite,
bila kutafakari kwa kina madhara watakayosababishwa na kipengele cha fao la
kujitoa.
Kufuatia hali
hiyo, wafanyakazi hao wa GGM walihoji uhalali wa sheria hiyo kuanza kutumika
haraka haraka bila kuwa na kanuni zake, na kwamba uharaka huo una siri ndani
yake.
Haule alihoji
pia sababu ya sheria hiyo kutowagusa wabunge, badala yake imetungwa kwa lengo
la wafanyakazi wengine, jambo alilodai limeonyesha ubaguzi mkubwa kwani wabunge
wanaruhusiwa kupewa mafao yao punde Bunge linapovunjwa na Rais.
“Hivyo
wafanyakazi walalahoi wanaamini kwamba sheria hii haina nia njema kabisa kwa
mstakabali wa maisha yao na vizazi vyao,” alisema.
Aidha
alitangaza kwamba mbunge yeyote atakayeonekana kushabikia au kupendekeza sheria
hiyo iendelee kutumika, wataunganisha nguvu zao kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao
mbunge huyo hachaguliwi tena.
Chanzo: Tanania Daima
0 comments:
Post a Comment