na Mwandishi wetu, Geita
SERIKALI mkoani
Geita imeanza mchakato wa kuhakikisha wachimbaji wakubwa wa dhahabu wanaohodhi
maeneo wananyang’anywa na kupatiwa wachimbaji wadogo.
Mkuu wa Mkoa wa
Geita Magalula, Saidi Magalula, alitoa kauli hiyo juzi katika taarifa yake ya
mkoa mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen
Wassira, mjini Geita.
Alisema kitendo
cha wachimbaji wakubwa kuchukua maeneo hayo bila ya kuyaendeleza kwa shughuli
za uchimbaji kimechangia migogoro ya mara kwa mara kati yao na wachimbaji
wadogo.
Kwa sababu
hiyo, alisema tayari uongozi wa mkoa kupitia Idara ya Madini, umeandika barua
kwenda Wizara ya Nishati na Madini ili kuomba kuchukua hatua ya kuyatwaa maeneo
hayo na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni moja ya njia za kupunguza
migogoro hiyo.
Magalula
alisema kila wananchi wanapogundua uwepo wa dhahabu katika maeneo mbalimbali
linaibuka kundi la wachimbaji wakubwa na kudai kumiliki maeneo hayo, lakini
wamekuwa wakiyahodhi tu jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi pia
kuchangia migogoro mingi katika sekta hiyo.
Hata hivyo,
alisema hatua ya serikali ya kutenga maeneo ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwa
kiasi kikubwa kutapunguza kama sio kumaliza changamoto hiyo na kuboresha mahusiano
kati ya wananchi na serikali yao, lakini pia kati ya wananchi, wawekezaji na
wachimbaji wakubwa.
“Hivi sasa
uongozi wa mkoa umeendelea kuwahimiza na kuhamasisha wananchi na wachimbaji
wadogo kujiunga kwenye vyama vya ushirika na saccos ili kurahisisha
kushughulikia changamoto zinazowakabili,” alisema Magalula.
Kwa upande wake
Waziri Wassira alisema njia pekee ya kuwasadia wananchi kunufaika na rasilimali
za madini ni kwa kuwatengea maeneo wachimbaji wadogo, hivyo kupunguza tatizo la
ajira kwa vijana.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment