na Victor Eliud, Geita
WAKAZI wa
vitongoji vya Katoma na Nyamalembo wilayani Geita, wamevamia ofisi za
halmashauri ya wilaya hiyo na kuvuruga kikao cha madiwani kilichokuwa
kikiendelea, wakilalamikia hatua ya mkurugenzi kuingilia kati madai yao ya
fidia, ili kupisha mwekezaji wa kampuni ya mgodi wa dhahabu wa Geita GGM.
Hatua hiyo
ilikuja baada ya wananchi hao ambao wengi wao ni wakulima kuokota barua
iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi huyo, Charles Kimaro, yenye
Kumb.Na.GDC/L.20/3/VOL.II/I ya Septemba 11, mwaka huu, kwenda kwa mkuu wa mkoa
wa Mwanza ya kumteua Ofisa Misitu na Ofisa Kilimo na Mifugo Wilaya ya Geita
kuwa mjumbe wa kuhakiki madai ya fidia ya wananchi hao.
Baada ya
kutinga katika ofisi hizo na kugundua kulikuwa na kikao hicho waliamua
kung’ang’nia kwenye lango kuu la ukumbi wa halmashauri hiyo wakishinikiza kutoa
malalamiko yao.
Kitendo hicho
kiliwalazimu madiwani kusimamisha kikao hicho kwa muda na kukutana na wananchi
hao ambao walidai Kaimu Mkurugenzi anatafuta maslahi binafsi kupitia migongo ya
wananchi wanyonge wanaotakiwa kulipwa fidia kupisha mgodi huo.
Walieleza kuwa
hawakubaliani na kitendo cha Kaimu Mkurugenzi huyo kuingilia kati suala hilo
kwa kuwa tayari lilishafanyika chini ya Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali na
kwamba hatua ya kiongozi huyo inalenga kuwakumbatia wawekezaji na kuwanyonya
wazawa.
Walidai kwa
mujibu wa ripoti ya mthamini mkuu wa serikali wanapaswa kulipwa sh bilioni
13.2, lakini mkurugenzi huyo anapinga na kushinikiza walipwe sh bilioni 8.2.
Kwa upande
wake, Ofisa Uhusiano wa mgodi wa GGM, Clement Msalangi, alisema hana taarifa za
kuwepo kwa malalamiko hayo na kwamba uongozi wa mgodi huo haujapokea barua ya
mkurugenzi wala uongozi wa mgodi haujapata nakala ya ripoti ya mthamini mkuu wa
serikali kuhusu fidia ya wakulima hao.
Akizungumzia
hilo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Daud Sweke, alisema suala hilo liko
kwenye mamlaka husika na kwamba ni kosa wananchi kuwa na nyaraka ya serikali
huku akitoa wito kwa wananchi hao kuvuta subira wakati suala hilo likiendelea
kushughulikiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment