na Victor Eliud, Geita
WAANDISHI wa habari mkoani Geita wamefanya maandamano ya amani kulaani mauaji ya mwaandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwagosi yaliyotokea Septemba 2.
Wanachama wa Geita Press Club (GPC) hawakuweza kufanya maandamano yaliyofanyika nchi nzima wiki iliyopita kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya uwepo wa ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mkoani Geita ambapo waandishi hao walikuwa katika ziara hiyo.
Akisoma taarifa ya chama kuhusu maandamano hayo, Mwenyekiti wa GPC, Victor Bariety, alisema klabu hiyo inaunga mkono kulaani kwa nguvu zote mauaji hayo na kuongeza kuwa mauaji hayo yamebadili sura ya Tanzania kimataifa kuwa kisiwa cha amani na sasa kuwa kisiwa cha mauaji.
Bariety alisema, pamoja na mtuhumiwa wa mauaji hayo, Pacificus Clephace kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji, lakini bado kuna watuhumiwa wengine ambao wanapaswa kuburuzwa mahakamani akiwemo Kamanda wa polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda.
Alisema kitendo cha serikali kukaa kimya dhidi ya watuhumiwa wengine wa mauaji hayo akiwemo Kamanda Michael Kamuhanda, ni kitendo cha kuzidi kupingwa siku zote hadi pale serikali itakapowakamata watuhumiwea hao.
Aidha, baadhi ya waandishi wa habari mkoani hapa walisema kutokana na viongozi wenye dhamana akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi kushindwa kuwajibika, Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuwachukulia hatua viongozi hao.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment